April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tulia Trust yawagusa wanafunzi wanaoishi mazingira hatarishi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WANAFUNZI wanaoishi katika mazingira hatarishi Jijini Mbeya wamepatiwa msaada wa madaftari na Taasisi ya Tulia Trust ikiwa ni mwendelezo wa kusaidia  jamii kwa  kata 36 zilizopo Jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo,Machi 12,2024 mara baada kukabidhiwa Daftari kwa shule ya msingi Hasanga,Uyole  pamoja na Kilimo iliyopo  kata ya Uyole Jijini Mbeya,Ofisa Elimu kata ya Uyole ,Mwl.Lucas Komba amesema kwamba msaada uliotolewa na Taasisi ya Tulia Trust utawapa bidii ya kusoma wanafunzi kwani awali walikuwa na mahudhurio hafifu darasani kutokana na kukosa vifaa vya kujifunzia.

“Awali watoto hawa walikuwa na mahudhurio hafifu lakini hivi sasa baada ya kupatiwa vifaa vya kujifunzia ikiwemo Daftari na sare za shule hivi sasa mahudhurio yao yamekuwa mazuri darasani  na hata utoro kupungua tunashukuru uongozi wa shule hii ya Hasanga kutoa taarifa za watoto hawa na kuona  umuhimu wa kusaidiwa na taasisi ya Tulia Trust “amesema Ofisa Elimu kata hiyo.

Kwa upande wake Ofisa habari na mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust,Joshua Mwakanolo amesema kuwa msaada uliotolewa kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni ahadi aliyoitoa  Spika wa bunge  na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt.Tulia Ackson wakati alipokabidhi sare za shule kwa wanafunzi 3000 mwezi January mwaka huu  ambapo ilitakiwa wanafunzi hao wapatiwe daftari lakini kutokana na kuchelewa kufika kwa daftari hizo Dkt.Tulia alitoa agizo kwa wanafunzi  wote wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatiwe   mara baada ya kufika vifaa hivyo vya kujifunzia kwa kata 36.

Akielezea zaidi Ofisa habari huyo amesema kuwa katika zoezi hilo jumla ya daftari 600000  zitatolewa kwa kata 36 za Jiji la Mbeya na kuwa zoezi hilo.litakuwa endelevu kwa mkoa wa Mbeya na adhima ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya  mjini Dkt.Tulia Ackson  nimekuona lengo lake linatimia la kusaidia wahitaji.

Hata hivyo Mwakanolo amesema kuwa  katika kata  ambazo wamekuwa wakipita wamekuwa wakikutana na changamoto ya watu wenye ulemavu huwapatia viti mwendo na Magongo yote ni  kuhakikisha kuwa  wanawaondolea adhima  wategemezi wao kwa kuwabeba mgongoni na kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Aidha Mwakanolo amesema vitimwendo  vitatolewa kwa kata 36 za Jiji la Mbeya na kuwa  kulingana na uhitaji watarajia kutoa  viti mwendo zaidi ya 36  kulingana na uhitaji na kuwa wahitaji ni wengi hawawezi kumaliza wote kwa wakati mmoja.

Aidha Mwakanolo ametaja shule walizofikia mpaka Sasa kuwa ni Mafanikio shule ya msingi ,Mwasote Shule ya msingi, Tambulika Reli Shule ya msingi,Uyole,Hasanga,Kilimo na kwamba lengo ni kufikia kata 36 zote za Jiji la Mbeya.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya msingi Hasanga ,Mwl.Alphonce Mkuchika amesema kuwa  shule ya Hasanga ina jumla ya wanafunzi 1,150 na wanafunzi waliopatiwa msaada ni 37 ambao ni kuanzia darasa la kwanza mpaka Darasa la saba nakushukuru kwa msaada huo na kusema watoto  hao baadhi yao walikuwa wanashindwa kuandika darasani kutokana na kukosa vifaa vya kujifunzia.