May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yakagua ujenzi jengo la Wizara ya Nishati Mtumba

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kushirikisha Taasisi za Umma katika utekelezaji wa mradi
wa ujenzi wa jengo la Wizara katika Mji wa Serikali-Mtumba na hivyo kuziimarisha katika utoaji wa huduma.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda ametoa pongezi hizo wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokagua ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma leo Machi 12, 2024.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa sita kutoka kushoto) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati wakikagua jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali-Mtumba jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2024.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, Naibu wake, Judith Kapinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Nishati walishiriki katika ukaguzi wa jengo hilo.

“Baada ya kufika hapa tumeona kuwa mkandarasi wa mradi huu ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mshauri Elekezi ni kampuni ya ABECC
ambayo ipo chini ya Chuo Kikuu Ardhi, Kamati inawapongeza kwa hatua hii ya kuzishirikisha Taasisi hizi za umma kwani pesa inayotolewa hapa na Wizara inarudi kuiimarisha mihimili mingine ya Serikali,” Amesema Ng’enda

Aidha, Ng’enda amezitaka Taasisi hizo zifanye kazi kwa kasi, weledi na kwa wakati ili kuwawezesha watumishi kuanza kutumia jengo
hilo kutoa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa Pili kutoka kushoto) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati wakikagua jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali-Mtumba jijini Dodoma tarehe 12 Machi 2024.

“Kwa kuwa mkandarasi umethibitisha kuwa fedha ya kutekeleza kazi hii unayo na unalipwa kwa wakati, hakikisha mnafanya kazi usiku na mchana na mhakikishe kuwa mafundi na vibarua wanalipwa pesa zao kwa wakati ili kuleta ufanisi kwenye kazi,” Amesema Ng’enda.

Vilevile, amemtaka mkandarasi kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika kwenye kazi ya umaliziaji wa jengo hilo vinapatikana kwa wakati ili kutochelewesha kazi nzuri ambayo imefanyika hadi sasa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda akizungumza wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipokagua ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma tarehe 12 Machi, 2024.

Awali, Msimamizi Kazi za Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Nishati, Alphonce Kilovere amesema mradi huo umefikia asilimia 75 ambapo
gharama ya mradi ni shilingi bilioni 25.2.

Aidha ameeleza kuwa, kazi ujenzi wa jengo hilo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

Muonekano wa jengo la Wizara ya Nishati baada ya kukamilika kwake katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma