May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yatekeleza agizo la Samia korosho kupitia Bandari Mtwara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Septemba 2023 la kutaka kusafirisha korosho za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Bandari ya Mtwara.

Katika kutekeleza agizo hilo tani 229,544 za korosho ghafi zimesafirishwa nje ya nchi kwa kutumia Bandari ya Mtwara katika msimu wa mwaka 2023/24, huku minada 55 ikifanyika nchini.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kijavara, kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo wa ushoroba wa Mtwara.

Alisema usafirishaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa. Alisema Katika kipindi hicho tani 244,680 za korosho ghafi zenye thamani ya Sh454 bilioni zimezalishwa nchini

“Bandari yetu imefanyiwa maboresho makubwa sambamba na kuongeza vifaa vyenye nguvu ili kufanya kazi kwa ufanisi na tumeleta mashine za kupakia na kupakua mizigo na kuongeza idadi ya wafanyakazi katika bandari hiyo,” alisema Kijavala.

Akiwasilisha taarifa ya msimu wa korosho, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Masoko na Udhibiti wa Ubora wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Revelian Ngaiza, alisema zaidi ya tani 244,680 zimezalishwa nchini na tani 144,018 zimekusanywa ndani ya Mtwara.

“Tulifanya zaidi ya minada 55 ya korosho ghafi nchi nzima kupitia vyama vya ushirika, zaidi ya tani 244,680 za korosho ghafi zilikusanywa na kuuzwa huku tani 229,000 zikisafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara ambazo zilitoka mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma,” alisema Ngaiza.

Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara viwanda na Wakulima, Kizito Galinoma, alisema mbali na maboresho yaliyofanikisha korosho kupita Bandari ya Mtwara kupitia ushoroba, wanaomba ujenzi wa reli uzingatiwe na bandari iboreshwe zaidi.

“Unajua bandari haikupitisha korosho kwa zaidi ya miaka mitano, kitendo cha kupitishia hapa kwetu ni faraja, pamoja na changamoto mbalimbali hasa vifaa lakini tuliweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Galinoma.