July 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THBUB yapongezwa, yaagizwa kukuza uelewa haki,wajibu

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuendelea kutoa elimu ya haki na wajibu kwa Watanzania kwa kuwa haki za binadamu haziwezi kutenganishwa na uwajibikaji wa kila mwananchi huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa wajibu wa kiraia ndiyo msingi wa kulinda haki hizo na kudumisha amani nchini.

Katimba ametoa kauli hiyo leo Julai 1, 2026 alipotembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Katimba amesisitiza kuwa kila Mtanzania anayefika katika banda hilo anapaswa kupewa elimu siyo tu kuhusu haki za binadamu, bali pia kuhusu wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Katiba yetu imehakikisha haki za binadamu zinalindwa, lakini pia kupitia Ibara ya 25-28 inaeleza wazi kuwa pamoja na haki, kila mwananchi ana wajibu wa kutimiza majukumu yake kwa manufaa ya taifa,” alisema Katimba.
Akizungumzia kuhusu uelewa wa wananchi, Katimba amesema changamoto iliyopo ni kwamba wananchi wengi wamekuwa wakifahamu zaidi haki zao kuliko wajibu wao, hali ambayo inaweza kuchangia uvunjifu wa sheria na migogoro isiyo ya lazima.

“Sasa watu hawaelimishwi vya kutosha kwamba haki zao za binadamu zinaenda sambamba na uwajibu wao. Unapokiuka wajibu wako kama raia, unaweza pia kuathiri ulinzi wa haki zako,” amesisitiza.

Aidha, Katimba amerejea Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayomtaka kila mwananchi kushiriki katika kuilinda nchi na kudumisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya Taifa.