July 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Chapo kufungua rasmi maonesho ya Sabasaba 2026

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) utakaofanyika Julai 3, 2026 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Rais Chapo ataambatana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika hafla hiyo ya ufunguzi rasmi.

Kapinga amesema maonesho ya mwaka huu yamevutia washiriki 3,722 kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku mataifa 23 yakishiriki kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na ubunifu mbalimbali.

Amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na kuhamasisha ongezeko la thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, sambamba na kuonesha mafanikio ya uwezeshaji wa wananchi kupitia mikopo na fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.

Kwa mujibu wa Kapinga, amesema.wananchi watapata nafasi ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wanawake na vijana baada ya kuongezewa thamani, hatua inayochangia kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa maonesho ya mwaka huu yanaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyoanza rasmi Julai 1, 2026, ikiwa na lengo la kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Aidha, amesema waandaaji wameboresha huduma kwa wageni ikiwemo kuweka magari maalumu yatakayowasaidia watu wenye changamoto za kutembea kwa umbali mrefu kuzunguka maeneo ya maonesho kwa urahisi.

Kapinga pia amesema Julai 6 kutafanyika hafla maalumu ya Golden Jubilee ya maonesho hayo, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi.