April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TET yakabidhi vitabu vya shule msingi na sekondari Muleba

Na Mwandishi wetu ,timesmajira, Muleba.

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) katika kuondoa upungufu wa vitabu kwa wanafunzi nchi, imekabidhi jumla ya vitabu 173,990 kwa ajili ya shule za Msingi na vitabu 2,714 kwa ajili ya shule za Sekondari, Wilayani Muleba, Kagera.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya vitabu hivyo, Mkuu wa Wilaya  ya Muleba, Toba Nguvila  amesema itasaidia kuondoa upungufu wa vitabu kwa wanafunzi huku akiwaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Ma-Afisa Elimu pamoja na Walimu wote kuhakikisha vitabu vinakwenda kutumika kama kusudio lilokusudiwa na Serikali.

Ambapo amewataka kuhakikisha wanakwenda kuwafanya wanafunzi kuwa na vitabu vya kutosha ili kupata elimu bora.

“Tunataka Wilaya ya Muleba iwe kinara wa elimu kwa maana ya ufaulu, kuongoza Kitaifa na inawezekana kwasababu tayari ,Rais ametupa vitabu kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania na nina amini vitabu hivi vinaenda kutumika kama vilivyokusudiwa,” ameeleza Mkuu wa Wilaya hiyo Nguvila.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa shule za Msingi, Mwalimu Severine Musyangi amesema kuwa vitabu hivyo vitasaidia  kupunguza uhaba uliokuwepo wa vitabu kwa wanafunzi. 

Amesema kwa sasa ujio wa vitabu hivyo utawezesha wanafunzi kupata kitabu kimoja kwa kila mwanafunzi mmoja.