April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tazama kijana aliyebuni mtambo wa kuzalisha gesi ya kupikia

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAONYESHO ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu yamemuibua kijana Paschal Massay kutoka chuo cha VETA Dodoma aliyetengeneza mtambo wa kuzalisha gesi kwa kutumia nishati ya mafuta ya petrol na maji.

Akizungumza na mtandao huu katika maonyesho hayo katika banda la VETA  jijini Dodoma Massay amesema,matumizi ya mtambo huo yatasaidia katika utunzaji wa mazingira kwani yatapunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Kijana huyo amesema,aliamua kubuni mtambo huo baada ya kuona gharama katika mkaa na gesi zinazotumika majumbani kuwa bei juu lakini pia baada ya kuona matumizi ya mkaa na kuni yanasababisha uharibifu wa mazingira.

“Hivi sasa vitu vimepanda bei ikiwemo mkaa na gesi ya kupikia majumbani,kwa nikaona miongoni mwa wanaopata tabu ni wajasiliamali wadogo wanaotumia nishati hizo hivyo nikaona mtambo huu utawasaidia,

“Mtambo huu pia utaondoa suala zima la uharibifu wa mazingira wa kukata miti ili kupata kuni kwa ajili ya matumizi ya kupikia.”amesema Massay

Amesema,mtambo huo ambao gharama yake ni shilingi 450,000 unatumia dizeli kidogo ambapo kwa siku mbili hadi tatu inaweza kutumika dizeli nusu lita.

“Tumefanya utafiti tumeona kuwa katika matumizi ya kila siku ya kupika ,nusu lita inakaa zaidi ya siku mbili kwa hiyo ni nafuu kwa matumizi tofauti na gesi za majumbani.”amesema Massay

Aidha ametumia fursa ya maonyesho hayo kuiomba Serikali kuwasaidia katika kuboresha bunifu zao ili ziwe katika ubora na viwango vinavyotakiwa ili ziweze kuingia sokoni na hatimaye vijana wabunifu waweze kujiajiri na kujipatia kipato.