April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yapiga hatua kibwa sekta ya Nishati

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

NAIBU  Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Tanzania inaendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya nishati, hususan matumizi ya nishati safi ya kupikia, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametunukiwa tuzo ya kimataifa kutokana na juhudi zake katika eneo hilo.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati, Makamba aMEsema Rais Samia ameendelea kuwa kinara wa mageuzi ya matumizi ya nishati safi, akilenga kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza muda unaotumika na wanawake jikoni.

Amesema Rais ameweka lengo kwamba ifikapo mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia, huku hadi sasa zaidi ya asilimia 28 tayari wameanza kutumia nishati hiyo.

“Wabunge wamemtendea haki Rais kwa kutambua kazi kubwa anayofanya katika sekta ya nishati safi ya kupikia. Hizi ni juhudi za dhati za kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira yetu,” amesema Makamba.

Amefafanua kuwa hadi sasa Serikali imefanikiwa kusambaza miundombinu ya gesi kwa zaidi ya asilimia 56.4 ya mabomba nchini, pamoja na kusambaza mitungi ya gesi zaidi ya 300,000, majiko banifu zaidi ya 49,000 na majiko ya umeme zaidi ya 7,000 katika maeneo mbalimbali.

Makamba amesema pia kumekuwa na maboresho makubwa katika taasisi, hususan shule za bweni, ambapo zaidi ya taasisi 53 zimepatiwa majiko ya nishati safi ya kupikia, hatua iliyoboresha mazingira ya upishi yaliyokuwa yakikumbwa na moshi na masizi.

Amewahakikishia wabunge kuwa katika bajeti ijayo, Wizara imepanga kusambaza majiko ya nishati safi katika taasisi zaidi ya 400 ili kuondoa matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wa umeme, Makamba alikiri kuwa changamoto bado ipo katika maeneo ya visiwa, lakini alisema hatua kubwa zimepigwa ambapo kati ya visiwa 143 vyenye wakazi, zaidi ya visiwa 120 tayari vimefikishiwa umeme wa sola, huku Serikali ikitoa ruzuku ya asilimia 45 hadi 75 kwa wananchi wa maeneo hayo.

Kuhusu matumizi ya gesi kwenye magari, alisema Serikali imeongeza vituo vya kujaza gesi kutoka tisa mwaka 2024/2025 hadi kufikia vituo 18 kwa sasa, na ina mpango wa kuanzisha mfumo wa mini mobile LNG ili kurahisisha upatikanaji wa gesi katika mikoa ambayo haijafikiwa na bomba la gesi.

“Lengo ni kuhakikisha Mtanzania anaweza kusafiri kwa kutumia gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kurudi bila changamoto,” amesisitiza.