April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msimu wa ununuzi wa ufuta Songwe ni Mei, miundo mbinu yaboreshwa

Na Moses Ng’wat, Songwe.

CHAMA Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (SORECU) kimetangaza kuwa msimu wa ununuzi wa zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani utaanza rasmi Mei 8 na 9, 2026, huku kikitangaza kuboresha huduma kwa wakulima na vyama vya msingi.

Hayo yalibainishwa, Aprili 23, 2026 na Meneja wa chama hicho, Daudi Slahhi, wakati wa mkutano wa jukwaa la wadau wa tasnia ya ufuta uliofanyika sambamba na ufunguzi wa msimu huo katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nselewa, Mlowo wilayani Mbozi.

Slahhi amesema kuwa katika msimu wa kilimo 2026/2027, chama hicho kimejipanga kukabiliana na changamoto zilizojitokeza msimu uliopita kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha wakulima wananufaika ipasavyo na mfumo huo, huku SORECU ikiongeza ufanisi katika ukusanyaji, uhifadhi na uuzaji wa zao la ufuta.

Akizungumzia kuhusu miundombinu ya maghala, Slahhi alisema idadi ya maghala imeongezeka hadi 12 katika msimu huu, ikilinganishwa na maghala tisa yaliyotumika msimu uliopita, hatua inayolenga kupunguza msongamano na tatizo la mazao kukaa nje wakati wa minada.

Alifafanua kuwa Wilaya ya Momba itakuwa na maghala matatu, huku Wilaya ya Songwe ikiwa na maghala tisa kwa ajili ya ukusanyaji wa mazao.

Aidha, alisisitiza kuwa matumizi ya mizani ya kidigitali yataimarishwa ili kuongeza uwazi na usahihi katika upimaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Fadhili Nkulu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, alisisitiza umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ghalani katika kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri, masoko ya uhakika pamoja na kuongeza thamani ya mazao yao.