April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

2030 Tanzania kifikia megawati 8,000 na megewati 70,000 ifikapo 2050

  Na Joyce Kasiki Timesmahira online,Dodoma

WAZIRI  wa Nishati, Deo Ndejembi, amesema kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kufikia uzalishaji wa umeme wa megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, huku malengo ya muda mrefu yakiwa ni kufikia megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050.

Ndejembi ameyasema hayo wakati akihitimisha hoja za wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati, akisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya nishati imejipanga kikamilifu kuhakikisha malengo hayo yanatimia.

Amesema serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, jua, upepo, makaa ya mawe na jotoardhi.

 Kwa upande wa miradi ya maji, Waziri alitaja maendeleo ya miradi kadhaa ikiwemo Mradi wa Maragarasi wenye uwezo wa kuzalisha megawati 49 ambapo mkandarasi tayari yupo site, Mradi wa Kakono (MW 87), Ruhudji (MW 358) pamoja na Rumakali (MW 222).

Aidha, Ndejembi amebainisha kuwa Tanzania inalenga kuzalisha megawati 130 kupitia nishati ya jotoardhi ifikapo mwaka 2030, huku pia ikiendelea kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha uzalishaji wa umeme wa megawati 2,000 kupitia makaa ya mawe.

Katika kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu, Waziri amesema kuwa tayari kuna mafanikio katika mradi wa umeme wa jua wa Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo megawati 59 tayari zimeingizwa kwenye gridi ya Taifa, na mipango inaendelea kuongeza megawati 100 zaidi kutoka eneo hilo.

 Ameongeza kuwa miradi mingine ya nishati ya jua inatarajiwa kutekelezwa katika maeneo ya Mbyuni na Zuzu, sambamba na miradi ya nishati ya upepo.

“Tumepanga kuhakikisha Taifa linakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hii yote inalenga kufikia megawati 8,000 ifikapo 2030 na hatimaye megawati 70,000 ifikapo 2050,” alisisitiza Ndejembi.

Aidha ameaema ,Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika unaochochea ukuaji wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.