NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukuza Kiswahili kama lugha ya kimataifa ya mawasiliano, elimu na diplomasia, akisisitiza kuwa lugha hiyo ni urithi wa pamoja unaochochea amani, mshikamano na maendeleo ya ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Mwijuma ametoa kauli hiyo alipowasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kilele cha Maadhimisho ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika jijini Bujumbura, Burundi leo Julai 7 ,2026. Katika salamu hizo, Mwinjuma ameipongeza Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) kwa juhudi zake za kuendeleza ajenda ya Kiswahili na kuimarisha nafasi yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa.
Akihitimisha kilele cha maadhimisho hayo, Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Jamhuri ya Burundi, Lydia Nsekela, amesema Kiswahili kimeendelea kuwa daraja muhimu la mawasiliano, na ushirikiano wa wananchi wa Afrika Mashariki na Bara la Afrika.
Hivyo amezitaka nchi wanachama kuongeza uwekezaji katika ufundishaji, matumizi na uendelezaji wa lugha hiyo ili kizazi kijacho kiendelee kunufaika na urithi huo.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), Dkt. Caroline Asiimwe, amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyofikiwa katika kukuza Kiswahili na kuweka mikakati ya kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kustawi katika elimu, teknolojia, biashara na diplomasia.
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hufanyika kila mwaka Julai 7 tangu yalipotangazwa na UNESCO mwaka 2021, hatua iliyokifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na kupewa siku maalumu ya kuadhimishwa duniani.

More Stories
Dkt.Samia:Kiswahili kifundishwe Duniani
Mpogolo: Hali ya usalama Ilala ni shwari
Mpogolo ataka TUGHE wachague viongozi wenye Maadili na Uadilifu