RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania Duniani, kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na kuanzisha vituo vya utamaduni wa Kiswahili katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Ufaransa.
Maelekezo hayo yamewasilishwa leo, Julai 7, 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASKIDU 2026) yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), jijini Paris, Ufaransa.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia, vituo hivyo vitakuwa kitovu cha kufundisha na kueneza lugha ya Kiswahili, kutangaza utamaduni wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla, pamoja na kuimarisha diplomasia ya utamaduni. Vilevile, vitafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kimataifa kupitia matumizi ya Kiswahili.
Aidha, vituo hivyo vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuwawezesha wananchi wa mataifa mbalimbali kujifunza historia, urithi, mila, desturi na ustaarabu wa Afrika kupitia lugha ya Kiswahili, ambayo inaendelea kupata hadhi na kutambuliwa katika majukwaa ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewahimiza Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kuhakikisha wanawarithisha watoto wao lugha ya Kiswahili ili kudumisha utambulisho wa Taifa, kuimarisha mshikamano wa kizazi hadi kizazi na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa Tanzania.
Amesisitiza kuwa kadri Kiswahili kinavyoendelea kupanua wigo wake duniani, ndivyo kinavyozidi kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushawishi wa Tanzania kimataifa, kukuza utamaduni wa Kiafrika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

More Stories
Tanzania kuendelea kukiinua Kiswahili Kimataifa
Mpogolo: Hali ya usalama Ilala ni shwari
Mpogolo ataka TUGHE wachague viongozi wenye Maadili na Uadilifu