July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tani 22.6 dawa za kulevya zakamatwa, 188 wanaswa

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata tani 22.6 za dawa za kulevya katika operesheni mbalimbali zilizofanyika nchini kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu.

Katika operesheni hiyo watuhumiwa 188 walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni za ndani na ushirikiano wa kimataifa uliowezesha kuvunja mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya.

Amesema, katika kipindi hicho DCEA ilikamata tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 11.63 za heroini, kilogramu 40 za skanka pamoja na lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya.

Aidha, mamlaka hiyo imeteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi katika wilaya za Chamwino mkoani Dodoma, Kilwa mkoani Lindi pamoja na Sengerema mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti uzalishaji wa dawa hizo nchini.

Lyimo amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ya operesheni hizo ni kukamatwa kwa tani 2.6 za mirungi katika eneo la Tarakea mkoani Kilimanjaro, zikiwa zimetokea Kenya na kusafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso kabla ya kukamatwa Mbezi Makonde, Dar es Salaam.

Amesema watuhumiwa kadhaa walikamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku mtu mmoja akitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na mtandao huo wa usafirishaji wa dawa za kulevya.

Katika operesheni nyingine zilizofanyika jijini Dar es Salaam, DCEA imekamata kilogramu 19.94 za bidhaa zilizokuwa zimefichwa katika vifungashio vilivyoonekana kuwa virutubisho vya lishe aina ya AFACELL (Moringa Extract).

Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa maabara kubainika kuwa zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya dawa za kulevya aina ya Prazepam.

“Bidhaa hizi ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zinaandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” amesema Kamishna Lyimo.

Ameonya kuwa, matumizi holela ya dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya kama Prazepam bila ushauri wa daktari yanaweza kusababisha uraibu, kuharibika kwa mfumo wa fahamu, matatizo ya upumuaji, kupoteza fahamu na hata kifo.

Aidha, amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), DCEA ilibaini uwepo wa baadhi ya vinywaji aina ya energy drinks vilivyokuwa na kemikali ya THC, ambayo ni kiambata kinachopatikana kwenye bangi na kina madhara mbalimbali ikiwemo kuathiri afya ya akili, mfumo wa fahamu na kuongeza vitendo vya uhalifu.

“Tumeimarisha ushirikiano wa kiutendaji na mamlaka za nchi za Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia na Kenya katika kukabiliana na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya,” amesema Kamisha Lyimo.

Amesema, operesheni za pamoja zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na biashara hiyo dawa za kulevya zitasikika kwenye bomba tu.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya ili kulinda afya, usalama na ustawi wa jamii.