July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Omar apongeza Juhudi za kulinda amana za wateja

:
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, leo Julai 2,2026  ametembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea jijini humo.

Katika ziara hiyo, Waziri Omar alipokelewa na viongozi pamoja na wafanyakazi wa DIB, ambapo alipatiwa maelezo kuhusu majukumu ya Bodi hiyo, huduma mbalimbali inazotoa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Mfumo wa Bima ya Amana.

Akiwa katika banda hilo, Waziri huyo pia alipata ufafanuzi kuhusu mchango wa DIB katika kulinda amana za wateja wa benki na taasisi za fedha, hatua inayochangia kuimarisha imani ya wananchi pamoja na uthabiti wa sekta ya fedha nchini na Waziri huyo alipongeza juhudi za Bodi hiyo katika kuwahudumia wananchi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Ofisa Mwandamizi wa DIB, Joyce Shala, amesema bodi hiyo imeongeza jukumu la kupunguza hasara katika utatuzi wa migogoro au changamoto zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa taasisi za fedha, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa sekta ya fedha.

Shala alisema DIB imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi, ikiwemo kufanikisha ulipaji wa fidia kwa wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME kwa kiwango cha asilimia 85. Alifafanua kuwa malipo hayo yalifanyika kwa awamu mbalimbali ili kuhakikisha wateja wanarejeshewa sehemu kubwa ya amana zao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aliongeza kuwa ushiriki wa DIB katika Maonesho ya Sabasaba unalenga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Amana, haki za waweka amana na nafasi ya bodi hiyo katika kulinda mfumo wa fedha wa nchi.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yamewakutanisha taasisi za umma na binafsi kutoka ndani na nje ya nchi, yakitoa fursa ya kuonesha huduma, bidhaa na ubunifu unaochochea maendeleo ya uchumi na biashara nchini.