May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yapongezwa utekelezaji thabiti miradi ya umeme nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limepongezwa kwa utekelezaji thabiti wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo midogo midogo na mikubwa ya kimkakati ambayo inawezesha usambazaji wa nishati hiyo nchini kote.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alipotembelea banda la TANESCO katika maonesho ya Teknolojia yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.

Sambamba na pongezi hizo, Mtaka ameshauri wataalamu wa Tehama wa TANESCO kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu ili kuboresha mifumo ya utoaji huduma ikiwemo huduma za ununuzi wa umeme wa LUKU ili kuwezesha wateja kununua umeme kisha umeme huo kuingie katika mita bila kumlazimu mteja kwenda kuweka umeme katika mita yake.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Kenneth Boimanda, wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipotembelea Banda la TANESCO katika maonesho ya teknolojia yanayoendelea katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo.

Mtaka alisema pamoja na mambo mengi mazuri ambayo TANESCO imekuwa ikiyafanya, ni vyema Shirika likafanya ushirika na taasisi za elimu ya juu ili kukuza ubunifu na kuwezesha wataalamu wa ndani kutumika katika kutekeleza miradi mbalimbali bila kuhitaji wataalamu kutoka nje ya nchi na ikiwezekana wataalamu wa Shirika waweze kufanya na kusimamia hata miradi mingine mikubwa inayotekelezwa katika nchi jirani.

“Hii nikutokana na uzoefu ambao wataalam wa TANESCO watakuwa wameupata baada ya kukamilisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema Mtaka

Mtaka ameongeza kuwa, miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kwa weledi wa hali ya juu, hivyo ni vyema sasa TANESCO ikawezesha wataalam wake kwa kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali kuanza kupeleka wataamamu katika kandarasi za usimamizi wa miradi nje ya nchi.