May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanesco Saccos watoa mashuka 300 Hospitali ya Ocean Road

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija amevitaka vyama mbalimbali vya ushirika kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za kuisadia jamii hasa katika kuboresha huduma za afya kwa kutoa vifaa tiba na dawa.

Hayo ameyasema jana jijini Dar es Salaam wakati wa kamabidhiano ya mashuka 300 yenye thamani ya shilingi milioni 11 yaliyotolewa na chama cha ushirika, Tanesco Saccos katika hospitali ya Ocean road.

“Saccos zingine zinatakiwa kuiga namna nzuri ya uendeshaji wa Saccos kwasababu hiki ni chama cha ushirika ambacho wameamua kuja kuisaidia jamii”

DC Ludigija amesema serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kufanya maboresho mbalimbali katika hospitali hiyo ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba hivyo amewataka Saccos kuendelea kutoa misaada mbalimbali katika hospitali ili kuboresha afya za akina mama, baba, vijana, wazee na watoto .

“Mashuka haya mliyoyatoa ni Msaada mkubwa sana kwenye hospitali hii ya ocean road ambayo serikali kupitia rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumefanyika maboresho makubwa kwenye hospitali hii na upatikanaji wa vifaa tiba lakini pia madawa”

Aidha amesema msaada waliioutoa Tanesco Saccos katika hospitali hiyo ya occean road itaongeza ari kwa watumishi na wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yao.

“Kwa namna wagonjwa tunaowapata hapa ocean road, mashuka haya yatawasaidia sana watumishi wetu katika kuwahudumia kwa ukaribu wagonjwa, kuwabadilishia nashuka mala kwa mala kwenye mazingira kama yale yanayofanana na nyumbani kwani ni tiba kubwa”

Kwa upande wake Mwenyewekiti wa chama cha ushirika wa akiba na mikopo – Tanesco Saccos Somoe Ismail amesema usambazaji wa vifaa hivyo walianza katika mkoa wa Mtwara, Kilimanjaro, Geita, na kwa sasa wapo Dar es Salaam katika hospitali ya Ocean road ambapo wanalenga kufanya hivyo kwa nchi nzima ili kuendelea kuboresha huduma za afya.

“Hii ni msingi kati ya misingi ambayo tunatakiwa kuifuata au kuitii hivyo tunawahamasisha washirika wengine na jamii kwa ujumla wajitokeza kutoa misaada ili kusaidia kuboresha afya za wenzetu”

Nao Wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali hiyo wamefurahishwa na msaada huo na kuwaomba mashirika mengine kuendelea kuwashika mkono ili waendelee kupata huduma bora hospitalini hapo.