April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMWA yampongeza Rais Samia kuendelea kuwaamini wanawake

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online,Dar

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuteua wanawake wawili katika Baraza la Mawaziri.

Uteuzi huo umefanyika juzi, ambapo Dkt Ashatu Kijaji ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati Dkt Stergomena Tax akiteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari,jana Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema uteuzi huo unafanya idadi ya mawaziri wanawake kufikia saba, kutoka watano walioteuliwa awali.

“TAMWA tunampongeza Rais Samia pia kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kumteua mwanamke kushika wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,”amesema na kuongeza;

“Uteuzi alioufanya Rais wa kuongeza mawaziri wawili katika baraza unaonesha dhahiri kuwa wanawake wanaaminika na wana uwezo wa kuleta mabadiliko katika nyanja zote, kisiasa, kiuchumi na kijamii,”amesema Dkt.Reuben

Dkt. Tax akiapishwa Bungeni, jijini Dodoma.

Amesema TAMWA inaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ndiyo nguzo muhimu ya kuleta usawa na ndicho chanzo cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii ambayo yataletwa katika usawa, haki na uwajibikaji.

“Rais Samia, ameweza kuonesha lile ambalo lilidhaniwa haliwezekani kwa kuwaweka mawaziri wanawake katika wizara nyeti kama ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, pia kwa kuendelea kuteua mawaziri wanawake, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala,” amesema Dkt Reuben

Aidha, amesema wanampongeza Rais Samia kwa kauli yake wakati akiwaapisha mawaziri hao jana , aliposema; “Nimeamua kuvunja taboo (mwiko), iliyoaminika kwamba wizara ya ulinzi lazima akae mwanaume mwenye misuli yake, kazi ya wizara ile si kupiga mizinga au kushika bunduki, nimevunja taboo (mwiko) hiyo na kumteua dada yetu Tax kutokana na upeo wake mkubwa alioupata akiwa Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara…”

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben

Amesema hakika Rais Samia amevunja dhana ya kuwa wanaume pekee ndiyo wenye uwezo wa kushika wizara hiyo na kwa hilo wanategemea Dkt. Tax hataweza kuwaangusha, bali atasimamia vyema nafasi hiyo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama kwa kuwa ana uwezo na upeo.

Amesema TAMWA inawapongeza Rais Samia kwa kusikiliza kilio cha wanahabari na kuunganisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na ile ya Teknolojia ya Mawasiliano kuwa moja.

“Hatua hiyo itawafanya wadau wa habari kufanya kazi kwa ufanisi na wepesi zaidi kuliko hapo awali, TAMWA tunaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na katika ngazi za maamuzi ndicho chanzo cha haki, usawa na uwajibikaji na maendeleo ya nchi,”amesema