September 25, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya afya Ileje yatumbua vigogo

Na Moses Ng’wat,timesmajira,Ileje.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, amewasimamisha kazi, Mganga Mkuu (DMO) wa Wilaya ya Ileje, Dkt.Janeth Makoye pamoja na Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Erick Rugeiyamu ili kupisha tuhuma zinazowakabili za matumizi mabaya ya fedha za miradi ya afya.

Huku amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kufuatia matumizi mabaya ya fedha za umma katika miradi ya Afya.

Mgumba amechukua hatua hiyo leo,  baada ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Igoye, Wilayani humo ambapo licha ya serikali kupeleka shilingi milioni 50, ujenzi wa Zahanati hiyo haujakamilika.

“Yaani leo nilipokuja hapa nilifikiri nitakuta ‘Madaktari na Manesi’ wapo na wananchi mnapata huduma, lakini baada ya kukagua jengo humu ndani, sitaki kuwa mnafiki sijafurahishwa,”Amesema na kuongeza

“Sijafurahishwa kwa kuwa mradi haujakamilika kwa wakati na nilipowauliza wataalamu wetu wameniambia sababu ni mvua barabara mbaya, lakini tangu nifike hapa Songwe mwezi wa tano hakuna siku hata moja mvua imenyesha,”amese,a

Amesema mradi wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Igoye ni miongoni mwa miradi ya afya katika Halmashauri hiyo ambayo imekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Amesema katika hali isiyokuwa ya kawaida licha ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 50 na wananchi kujitolea nguvu kazi yenye thamani ya shilingi milioni 19 bado ujenzi wa Zahanati hiyo ya kijiji imeshindwa kukamilika.

“Haiwezekani wananchi wajenge hadi kuezeka kwa kutumia shilingi milioni 19 alafu serikali ikaunga mkono kwa shilingi milioni 50 mnaniambia mmeshindwa kukamilisha ujenzi hapa kuna matumizi mabaya hivyo naagiza ndani ya siku saba takukuru mnipatie taarifa” amesema

Mbali na maagizo hayo, Mgumba ametoa siku saba kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana rushwa mkoa wa songwe kumpatia taarifa ya uchunguzi juu ya matumizi mabaya ya fedha katika Halmashauri hiyo.

“Na kwa mamlaka niliyopewa, ofisi yangu pia itaunda kamati maalum ya uchunguzi ili ikifikia wakati wa kuchukua uamuzi tusimuonee wala kumpendelea mtu” alisisitiza Rc Mgumba.  

Awali akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa Zahanati hiyo, Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Zahanati hiyo ya kijiji, Ephes Kibona, amemlalamikia kutishiwa maisha na baadhi ya watendaji wa Halmashauri kutokana na msimamo wake wa kutaka taratibu zifuatwe kwenye ujenzi.