April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamasha la Hip Hop Asili 2022 kuwakutanisha wasanii wa ndani na nje ya nchi

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

WASANII Mbalimbali kutoka Kenya, Ghana, Ufaransa na Marekani wanarajiwa kuungana na wasanii 36 waliochaguliwa katika Mashindano ya Hip Hop kutoka katika mikoa sita ya Tanzania katika Tamasha la muziki wa Hip Hop Asili 2022 awamu ya pili linalotarajiwa kufanyika kuanzia leo Juni 23 hadi Juni 25 katika ukumbi wa Alliance Francaise Jijini Dar e s Salaam.

Tamasha hilo ambalo litafanyika kwa siku tatu limeandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa Nchini Tanzania kwa kushirikiana na Wepresent Tanzania ambapo vijana wenye vipaji watapata fursa kuonesha vipaji vyao sambamba na kutoa burudani ya aina yake kwa waudhuriaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui amesema kuwa, tamasha hilo litawaweka vijana pamoja na kuwakilisha mawazo yao kupitia sanaa pamoja na kujitangaza.

Amesema Tamasha hilo litatoa burudani zenye utamaduni wa Hip Hop Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuonesha sanaa mbalimbali kama uchoraji, uimbaji Breakdancing, emceeing, Deejaying , Beat Boxing pamoja na skate boarding.

“Tamasha hili ni muendelezo wa tamasha lililofanywa na baadhi ya wana Hip Hop 30 wa Afrika Mashariki na Ufaransa Octoba Mwaka jana wa mkutano wa new African _France Summit (NSAF) ambao ulichochea kuandaliwa kwa mkakati wa ushirikiano wa Hip Hop kwa bara la Afrika kwa kipindi cha 2022/24″amesema

Amefafanua kuwa mwaka huu Tamasha litapambwa na wasanii Octipizzo kutoka Kenya, Tina Mweni (Kenya, Denmark), Rise up Band(Tanzania, Ufaransa), Jay Moe(Tanzania), The Mc 225 (Tanzania), Mic Crenshaw .(US), Lord Eyes( Tanzania) “amesema Balozi

Nakuongeza kuwa
“Wasanii kutoka nchi ya Kenya, Uganda, Rwanda , Burundi, Kongo, Ghana, Mayotte, Ufaransa na Marekani wataungana na wasanii wengine 36 waliochaguliwa katika mashindano ya Hip Hop Asili kutoka katika mikoa sita”amesema Balozi Hajlaoui

Ameongeza kuwa Juni 24 kupitia tamasha hilo kitakuwa na shindano la Break Dance la Afrika Mashariki ili kupata bingwa wa Tanzania ambaye atakwenda kwenye Battle of the year 2022 Tokyo Japan.

Aidha amesema kupitia tamasha hilo watarajia zaidi ya watu 1500 kuhudhuria ili kupata burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wenye vipaji vya asili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha utamaduni cha Alliance Francaise Frola Valleur amesema kuwa, tamasha hilo limelenga kujenga ushirikiano pamoja na kutangaza sanaa na tamaduni za Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla ulimwenguni.

Naye Mkurungezi wa miradi wa Tamasha la Festival Hip Hop Asili , Matei Babu amesema walifanya usaili wa kutafuta vijana wenye vipaji ambao watashiriki katika jukwaa moja na wasanii kutoka nje ya nchi.

Akitaja mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es salaam pamoja na Zanzibar.

Amesema wasanii hao waliopatikana katika usaili watapewa mafunzo ya siku tatu ambayo tayari yameishaanza na yanatarajia kukamilika Juni 22.

“Kupitia warsha hizo wasanii watapata maudhui ya historia ya Hip Hop Tanzania, Sanaa ya Emcee, Breakdance pamoja na Beat box na muwezeshaji atakuwa Bbyo Lilou kutoka Ufaransa ambaye ni Bingwa wa dunia wa breakdance, mwingine Deejay PH kutoka Ufaransa, Mejah Mbuya kutoka Tanzania”amesema Babu

Mkuki Byoga ni Mwenyekiti wa bodi ya Alliance Francise ambao ni wenyeji wa Tamasha amesema Tamasha hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na kuwauganisha vijana katika jukwaa moja kuonesha sanaa mbalimbali .

Katika Tamasha hilo kutakuwa na tiketi za aina mbili ambazo zitapatikana kwa shilingi 20000, na 10000.