April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM wakubali upatikanaji katiba mpya,ni kwenye kikao cha NEC

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa, itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka
amesema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambae pia ni  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo Juni 22, 2022 katika Ukumbi wa (White House) Makao Mkuu ya CCM Jijini Dodoma ikiwa ni utaratibu wa vikao vyake vya Kitaifa.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana jana  Ikulu Chamwino, Dodoma kwa kikao cha siku moja cha kawaida na ambapo kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilifanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura  Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele.

Ambapo Shaka amesema vikao hivyo vyote viwili vimejadili masuala mbalimbali ya msingi na kwamba  pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na Mameya .

Shaka amesema hayo jijini hapa leo ambapo amesema uteuzi huo ni Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji-Erasto B. Mpete
,Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
-Mohamed Festo Bayo na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi- Stuart Nathaniel Nkinda, Apaikunda Ayo Naburi na Zuberi Abdallah Kidumo.

“Pamoja na mambo mengi yaliyozungumzwa Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Ndugu Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele,”amesema Shaka.

Pamoja na hayo Shaka amesema kuwa miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Amesema Chama kimeishauri serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na kutaka  mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.

Licha ya hayo ameeleza kuwa  Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.

“Halmashauri kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo, Chama kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote,”amesema

Pia Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao.

Hata hivyo Shaka amesema Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana kuwa  upatikanaji wa Katiba Mpya na kwamba  Chama hicho kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kuishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya watanzania wote.

Pamoja na mambo mengine amezungumzia  masuala ya uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama,ambapo amesema Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya Kata/Wadi.

“Chama kimetakiwa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika ngazi hizi ili kuimarisha ushiriki wa haki, usawa na demokrasia katika ngazi zote zinazofuata kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi ya Chama,”amesema