April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB, RC Ibuge wateta mkakati kuinua kilimo Ruvuma

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Ruvuma

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wamekutana na kufanya mazungumzo ya namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya ufuta, alizeti na soya ili kuchochea zaidi ukuaji wa uchumi na kukuza hali za kimaisha kwa wakulima mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Brigedia Ibuge mbali ya kupongeza juhudi zinazochukuliwa na TADB katika kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji hapa nchini, ameiomba benki hiyo kuongeza uwekezaji wake katika mkoa huo ambao ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao.

Zao la ufuta

“Nichukue nafasi hii kuipongeza sana TADB kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuinua sekta ya kilimo ikiwemo ndani ya mkoa wa Ruvuma ambao umeweza kunufaika kwa kupata mkopo wa zaidi ya sh. bilioni tisa kutokana na miradi mbalimbali katika maeneo ya Madaba, Namtumbo na Songea,” amesema Brigedia Ibuge.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema mpaka sasa mkoa wake umeshachukua hatua kadhaa ikiwemo kufanya tafiti kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kama sehemu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya soya, alizeti na ufuta.

“Mbali ya miradi iliyofanywa na TADB katika sehemu mbalimbali za mkoa wa Ruvuma, mkoa umeona haja ya kuongeza uzalishaji wa mazao kama soya ambayo soko lake ni la uhakika kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Tanzania na China ya kununua soya ya Tanznaia kwa miaka mitatu,” amesema.

Aidha ameongeza kuwa mazao kama ufuta na alizeti yamekuwa na ustawi mzuri katika mkoa huo kutokana na tafiti zilizofanywa na hivyo kuwa na uwiano sawa na mikoa ya Singida na Dodoma.

“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wadau wa alizeti hivi karibuni mkoani Singida alisema Tanzania huagiza tani 400,000 kwa mwaka kufidia upungufu wa mafuta ya kula ambayo hugharimu zaidi ya sh. bilioni 474.

Gharama hizo tunaweza kuzipunguza au kuondoa kabisa kwa kuwekeza vya kutosha kwenye uzalishaji wa mazao ya mafuta ya alizeti na ufuta ambayo yanastawi vyema Ruvuma,’’ ameeleza.

Kwa upande wake, Justine amesema benki yake mpaka sasa imetoa mikopo ya moja kwa moja wa jumla ya sh. bilioni 3.14 na sh. bilioni 5.9 kutoka kwenye mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo ambapo mikopo hiyo imetumika kuwakopesha wakulima matrekta, ujenzi wa viwanda vya mazao ya mahindi na alizeti pamoja na pembejeo za kilimo.

“Mpaka sasa tumetoa zaidi ya sh.bilioni tisa na kupitia maombi ya Mkuu wa Mkoa ya kuimarisha mazao ya alizeti, soya na ufuta, TADB itatenga pia fedha itakayosaidia kuwawezesha maofisa ugani,” amesema.