May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kusaidia vijiji vilivyokubwa na mafuriko Karatu

Na Sophia Fundi, Timesmajira, Karatu

WANANCHI kutoka vijiji kumi (10) kata ya Karatu wilayani Karatu mkoani Arusha, wameiomba serikali kuwasaidia kufuatia mafuriko yaliyosababishwa wananchi hao kuzikimbia nyumba zao baada ya nyumba hizo kuzingirwa na maji.

Nyumba hizo zimemezwa na maji baada ya bwawa lililoko kujaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kutapika maji nje ya makazi ya watu, hivyo wameiomba serikali kutuma wataalam kuona jinsi gani ya kutoa maji hayo.

Hata hivyo wamemshukuru mbunge wa Jimbo la Karatu, Daniel Awack kwa msaada aliowapa wa chakula baada ya kupata kadhia hiyo ambayo imesababisha hasara kubwa huku wakiwa hawana makazi na chakula.

Mbunge Awack, ametoa msaada huo hivi Karibuni baada ya kutembelea maeneo ya watu yaliyoathirika ikiwemo eneo la bwawani na kujionea hasara kubwa iliyosababishwa na mafuruko.

Aidha, Wananchi hao wametoa kauli hiyo baada ya kupokea msaada wa mahindi kutoka kwa mbunge huyo zaidi ya magunia 200 yenye thamani ya shilingi milion 13.

Akizungumza na wananchi, mbunge huyo aliwataka wananchi hao kuwa wavumilivu katika kipindi hichi kigumu kwao kwani serikali iko pamoja nao huku akisema kwa kiasi alichotoa ni awamu ya kwanza ya msaada wake kwa wathirika hao.

Mbali na hivyo pia, ameahidi kuwasiliana na mamlaka zinazohusika kuhakikisha kaya zaidi ya 740 zenye watu zaidi ya 2463 zinapata msaada ikiwemo makazi ya kuishi.

Baadhi ya wazee waliohojiwa na mwandishi wamesema hali hiyo haijawahi tokea.

“Sijawahi kuona mafuriko Kama haya kwa Karatu nyumba zaidi ya 700 kumezwa na maji si Jambo la kuchekelea kwa baadhi ya watu kusema watu wamefuata maji siyo maji yamefuata watu.

“Angalia kwa Sasa haya maji yameshindwa kutoka yanazunguka tu kwenye makazi ya watu na mwisho wake Nini?. Tunaomba serikali itume wataalam kuona ni kwa jinsi gani maji haya yanaweza kutoka ili tupate hata baadhi ya vitu kwenye nyumba zetu ikiwemo mabati na tupunguze hata hasara,” amesema mmoja wa waathirika aliyejulikana kwa jina la Ramadhani.

Mbunge wa Jimbo la Karatu Daniel Awack (mwenye suti kushoto) akikabidhi msaada wa mahindi zaidi ya magunia 200 kwa katibu tawala wa wilaya kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani Karatu.