April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB kuwaptia mikopo wakulima wa zabibu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imewahakikishi wakulima wa zao la zabibu kupata mikopo itakayosaidia kuongeza uzalishaji na mnyororo wa thamani ya zao hilo, ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano na wadau wa zao hilo ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi jijini hapa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Japhet Justine, amesema benki yake itaendelea kutekeleza mikakati ya serikali ya kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo, ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji na kuwaunganisha wakulima wengi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao.

“Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa benki hii ni pamoja na kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mapinduzi yenye tija kwenye sekta ya kilimo nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo. Tunawahakikishia wakulima wa zabibu mikopo yenye masharti nafuu na ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu,’’ amesema.

Justine amewataka wakulima kuondoa hofu ya kukosa mikopo kwa kigezo cha kukosa dhamana, kwani kinachomfanya mkulima akopeshwe na benki hiyo ni uwezo wa mradi husika.

“TADB huwa tunatumia dhamana kama sehemu ya kupunguza makali pale ambapo deni litakaposhindikana kulipwa, hivyo nawaomba wakulima kuacha kufikiria juu ya dhamana,’’ amesema.

Ameishukuru serikali kwa namna ilivyorahisisha zoezi la upatikanji wa mikopo kupitia TADB kwa kutoa fedha kiasi cha sh. bilioni 55 kama sehemu ya dhamana, ili kumrahisishia mkulima mdogo aweze kukopesheka na benki pamoja na mabenki washirika.

“Tunaishukuru serikali kupiti Ofisi ya Waziri Mkuu ilipoona wakulima wadogo na wa kati wanashindwa kufikia asilimia 50 ya dhamana, ikatoa kiasi cha dola za Marekani milioni 25 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 55 za Kitanzania, ambapo kupitia TADB wanaweza kudhaminika na mabenki washirika,’’ amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Dkt. Geofrey Mkamilo amesema kuna upungufu katika uzalishaji wa miche ya zababu na kwamba wataendelea kufanya tafiti za mbegu bora zaidi na kuzizalisha kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya ndani.

“Tumeweka mkakati wa kuendelea kuzalisha miche bora kwa njia ya tone na chupa, ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa mbegu ambapo kwa Dodoma pekee zinahitajika takribani miche bilioni 5.6 zitakazopandwa kwenye eneo la hekta milioni 2.1, ambazo zinafaa kwa kilimo cha zabibu,’’ amesema Dkt. Mkamilo

Awali wakati akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wadau na taasisi zote zinazojihusisha na sekta ya kilimo ikiwemo TADB, TARI na Asasi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo (PASS) kuendelea na kampeni iliyoanzishwa na serikali ya kuhimiza kilimo cha zabibu kwa kumsaidia mkulima kuanzia maandalizi ya shamba, upatikanaji wa pembejeo hadi hatua ya mauzo.