April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi za elimu chini ya COSTECH zapongezwa kwa ubunifu

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online,Dar

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Taasisi za Elimu nchini ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) zimekuwa na ubunifu unaolenga moja kwa moja kutatua changamoto katika jamii.

Profesa Ndalichako, alisema hayo jana mara baada ya kutembelea banda la COSTECH katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema COSTECH imekuwa ikiendeleza wabunifu kila mwaka, kwani kumekuwa na mashindano na wale washindi wamekuwa wakiendelezwa kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

“Zile madharia ambazo zinafundishwa zinaenda mbali wanaweza kufanya vitu kwa vitendo ambavyo moja kwa moja vinaenda kugusa katika kujenga ujuzi unaomwezesha mtu kujiajiri au kuajiriwa katika sekta ambazo zinagusa changamoto za Watanzania,” alisema Prof.Ndalichako.

Pia, Profesa Ndalichako alitoa wito kwa wabunifu hasa wale ubunifu wao umefika mbali kuwasiliana na COSTECH kupitia mitandao ya kijamii ama kufika katika ofisi zao ili ubunifu wao utambuliwe na kuweza kusaidiwa kupitia kambi za atamizi ambazo ziko COSTECH.

Alisema katika ubunifu nyingi ambazo ameziona zinalenga katika kutatu matatizo ya kijamii, kwa hiyo anatoa wito kama kuna changamoto ya kimasoko, washirikiane na Wizara ya Viwanda na Biashara waone ni namna gani wanaweza kuwasaidia.

“Hii itasaidia kuwatangaza zaidi ili waweze kupata wateja wengi na biashara zao au ubunifu wao uweze kwenda kutoa mchango kwenye taifa letu”, alisema Profesa Ndalichako.