April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taaluma ya maendeleo ya na ustawi wa jamii ijikite kuimarisha msingi wa watoto

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema, taaluma ya maendeleo na ustawi wa jamii lazima ijikite kwenye kuimarisha msingi wa watoto kuanza safari ya ustawi wa maisha yao tangu kabla ya kuzaliwa,baada ya kuzaliwa ,kukuza hadi kufikia utu uzima ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa kwa tija.

Dkt.Gwajima ameyasema hayo Jana jijini hapa alipotembelea nyumba ya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu maarufu kama Kijiji Cha Matumaini kilichopo jijini Dodoma.

“Hatuwezi kuvumilia kuona watoto ambao katika kipindi wanachotakiwa wawe shule wao wanakuwa hawapo shuleni, katika kipindi wanacho takiwa wawe na wazazi wao wapate upendo wa jamii yao unakuta wapo wanahangaika mtaani, hili halikumpendeza Rais Samia Suluhu Hassan, ndio maana akaamua kuunda Wizara hii hivyo dhamana iliyopo mbele yetu nikuhakikisha tunafanikisha kukinusuru kizazi hiki” amesema Dkt. Gwajima.

Aidha Dkt. Gwajima amekipongeza kituo hicho kwa jitihada zake za kulea watoto hao kuanzia wakiwa wadogo hadi kufikia umri wa utu uzima.

“Nimekuwa nikisikia   Kijiji cha Matumaini ni mojawapo ya vituo vilivyofanikiwa sana katika huduma ya malezi na makuzi ya watoto waishio kwenye mazingira magumu .”Alisema na kuongeza kuwa

“Kituo kina watoto wachanga, wanaosoma chekechea, shule ya msingi, sekondari, vyuo vya kati, vyuo vikuu na wengine walishamaliza shule wanaendelea na maisha yao. “

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mwanaidi Khamisi, amesema ziara hiyo ni mwanzo wa kwenda nchi nzima kwa ajili ya kuyafikia makundi yote, ikiwepo Wanawake, Wazee na watu Wenye ulemavu, hivyo akatuma salamu kwa maafisa ustawi wa jamii kujiandaa kwani Dodoma ni Mwanzo wa safari ndefu ya matumaini.

Naye katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Zainab Chaula, amekipongeza Kijiji hicho kwa kuzingatia usawa wa kielimu, ambapo alisema miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kitaaluma kwenye mkoa wa Dodoma, ni St. Maria De Mathias, ambayo mbali ya kuwahudumia watoto wa kituo hicho vilevile hupokea watoto kutoka nje ya kituo.

Awali akisoma Risala ya kituo hicho mtoto Apia Aveline, aliyelelewa katika kituo hicho na kusoma hadi kufikia ngazi ya Utabibu, alisema wanakishukuru kituo hicho kwani zimefanikisha ndoto zao kuwa kweli, huku akiiomba Serikali kwa niaba ya Kituo kuangaliwa uwezekano wa kupata msamaha wa kodi wa vifaa vyao vinavyo ingizwa nchini, jambo ambalo Waziri alisema amelichukua na kuahidi kulifanyia kazi.

Kijiji cha Matumaini kilianza mwaka 2002 kikiwa na watoto watatu lakini kimeendelea kukua na kufikia  watoto 145 wakiwemo wavulana 62 na waschana 83 watoto hao wanaishi kwenye Nyumba 13 kwa mtindo wa kifamilia, ambapo kila nyumba kuna watoto wa umri tofauti na kutunzwa na Baba na Mama walezi wa kujitolea.