May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Siku za watumishi wabadhirifu zinahesabika’ Mchengerwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amewatahadharisha viongozi katika Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambao ni wazembe, wasio na nidhamu na wabadhilifu kuwa siku zao zinahesabika.

Akichangia hoja ya taarifa za kamati tatu za Bunge kuhusu ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG) Mchengerwa alisema:” wale wote waliotajwa kwenye ripoti naomba kusema maneno yafuatayo; ole wake kiongozi yeyote mzembe, asiye na nidhamu na mbadhilifu  kwenye wizara yangu na nitakayemkuta huko naomba niwaambie siku zao zinahesabika.”

Kauli ya Mchengerwa iliamshamshangwe kutoka kwa Wabunge huku wakigonga meza.

Aidha, Mchengerwa alimuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Nduguru kuchukua hatua dhidi ya Mkurugenzi wa Igunga ambaye alikua Mkurugenzi Kigoma Manispaa, Athuman Msabila kumsimamisha kazi mara moja kwasababu ya ushiriki wake wa fedha za mifumo akishirikiana na watendaji wa mifumo walioko Ofisi ya Rais Tamisemi waliotajwa.

 “WATU HAWA WASIMAMISHWE KAZI MARA MOJA.”

Aidha, Mchengerwa amesema tayari wizara yake imeanza kutekeleza taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kwa kuchukua hatua mbalimbali kwa wakurugenzi wa halmashauri zikiwemo za kuwasimamisha kazi, kutengua uteuzi na kuwafikisha mahakamani.

” Serikali ya awamu ya sita inachukia hatua madhubuti za kupambana na wabadhilifu wa fedha za umma kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa.”

Amesema wamewasimamiasha kazi watumishi walioshiriki kwenye ubadhirifu wa fedha za Serikali katika Halmashauri mbalimbali na kuchukua hatua kwa wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali ikiwemo wa Jiji la Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Arusha.

“Na hata aliyekuwa Mkurugenzi wa Sumbawanga akahamishiwa kwengine tumemrejesha ili akajibu kesi iliyoko mahakamani. Zile taarifa kuwa kuna watu wanahamishwa, katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita ya Dk.Samia Suluhu Hassan mtumishi yeyote popote alipo awe amehamishwa, awe amestaafu, atakayeshiriki kwenye ubadhilifu wa fedha za umma hatutasita kumchukulia hatua na huo ujumbe tumeshautuma.”

“Hapa tunavyozungumza wataalam wangu wako uwandani kuchunguza taarifa ambazo tumeendelea kuzipokea kutoka kwa watoa taarifa mbalimbali. Kwa Sasa tunaendelea na uchunguzi katika Halmashauri za Kibaha, Kigoma, Uvinza, Ileje na Ifakara.”

Alisema pia wameshachukua hatua ya kuwaondoa wakuu wa vitengo vya manunuzi na ugavi 23, wahasibu 16, wakuu wa vitengo vya rasilimali watu 6 na wakaguzi wa ndani wawili, waganga wakuu wa mikoa 10 na waganga wa Wilaya 46.

“Taarifa hii ya LAAC iwe kengele ya kutuamsha kila mmoja tutahakikishe tunawatendea haki watanzania. Serikali inafanya kazi kubwa sana ni lazima tumtendee haki Mheshimiwa Rais kwa sisi viongozi kufanyakazi kwa bidii kila mmoja katika eneo lake.”

“Wabunge wasisite kubainisha popote wanapoona changamoto, Tamisemi tutakuwa nanyi Leo na kesho kuhakikisha tunafanya kazi kwa ajili ya Watanzania.”