May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Silaa avalia njuga zoezi la utatuzi migogoro ya ardhi Dodoma


Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dodoma

Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameanza rasmi kambi ya Wiki mbili Jijini Dodoma kwa lengo la utekelezaji rasmi Maagizo ya CCM kuhakikisha Wizara yake inamaliza migogoro ya Ardhi katika Jiji la Dodoma.

Waziri Silaa mapema leo amezindua Kliniki ya Ardhi ambayo inawakutanisha wataalamu wote wa sekta ya ardhi na wananchi kwa lengo la kuhakikisha changamoto ya sekta ya ardhi katika Jiji la Dodoma inakwisha.

Akiongea na vyombo vya habari mapema leo tarehe 04/11/2023 wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo Silaa amewataka watendaji wote kuwa nje ya ofisi kuwahudumia wananchi katika zoezi ambalo pia yeye atashiriki kuongea na Wananchi bila wanachi hao kuweka miadi ya kuonana naye.

Aidha Waziri Silaa amewataka watendaji sekta ya Ardhi kuongeza jitihada pamoja na kuongeza kasi ya utendaji na kuongeza kuwa atakuwa akikutana na wananchi kila saa saba na kuhakikisha maelekezo yake yanayafanyiwa kazi.

Waziri Silaa amewataka maafisa wote wa Wizara yake kutoka maofisini kuwasiliza wananchi na kutoa suluhisho kwa changamoto zao za ardhi hasa wakati huu wa kliniki ya ardhi.

Tumeamua kuja hapa hadharani hakuna kificho hakuna mtu anayeweza kusema Afisa sikumkuta ofisini ili maafisa wote walioko halmashauri ya jiji na walioko kwa kamishna msaidizi wawe hapaAliongeza Jerry Silaa Waziri wa Ardhi.

Pamoja na jitihada hizi Waziri huyo amesema Wizara yake inakusudia kujenga ofisi za Kisasa za Sekta ya Ardhi Jijini Dodoma ambazo zitasanifiwa kwa ajili ya kuweka uwazi kwenye huduma za ardhi.

Mbali na kliniki hiyo Waziri Silaa amebainisha wazi kuwa tayari Ofisi ya Mkurugenzi wa halmshauri wa Jiji la Dodoma imetenga kiasi cha fedha za kitanzania Bilioni 4.5 kwa ajili ya fidia kwa ajili ya wananchi ambao maeneo yao yalighubikwa na changamoto katika zoezi la kupanga na kupima na kumilikisha Ardhi.

Kliniki hii inafanyika kwa mara ya pili sasa hapa Jijini Dodoma kwa lengo la kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kufanya utatuzi wa migogoro ya ardhi na ugawaji wa hati miliki za ardhi zoezi litakaloendelea kwa Wiki mbili.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry William Slaa akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi katika Ofisi ya Kamishna wa ardhi Dodoma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry William Slaa akisikiliza kero ya mteja wa kwanza kufungua huduma za pamoja za utatuzi wa migogoro alipofika kupata huduma katika banda la Wizara hiyo Jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi kutoka wizara ya Ardhi wakiendelea na zoezi la utoaji huduma ya Kiliniki ya Ardhi kwa wanachi wanaofika katika banda la Wizara hiyo.