April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka waajiri kutumia fursa ya msamaha wa tozo uliotolewa na NSSF

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Kagera

SERIKALI kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, imewaomba waajiri wote nchini, kutumia fursa adhimu iliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya kutoa msamaha kwa waajiri wote wenye malimbikizo ya tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango.

Waziri Jenista amesema hayo wiki hii alipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa pamoja na kuangalia shughuli za NSSF zinazofanywa kiwandani hapo ikiwemo uwasilishwaji wa michango

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (katikati) akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wahandisi wa kilimo katika kiwanda cha sukari Kagera, alipotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Kulia ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif na kushoto ni Mbunge wa Nkenge, Florent Kyambo.

Amesema msamaha huo umeanza Oktoba 1, mwaka huu na unahusu waajiri wote wenye malimbikizo ya michango na tozo kwa kipindi kinachoishia Juni 30, 2021 kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.

“Niwaombe waajiri watumie hii fursa iliyotolewa na NSSF, kwani huu ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kila siku anatafuta mbinu ambazo zitarahisisha shughuli za uwekezaji nchini,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akipata maelezo kuhusu mradi wa shamba la miwa Kagera wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha sukari Kagera. Kushoto ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif.

Waziri Jenista alisema waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango kuanzia mwezi huu Oktoba, 2021 mpaka Novemba 31, 2021 watalipa msamaha wa tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango husika kwa kiwango cha asilimia 100 jambo ambalo ni fursa kubwa kwa waajiri hao.

Alisema waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango ifikapo Disemba 31, 2021 watapa msamaha wa tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango husika kwa asilimia 75 na waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango ifikapo 31 Januari, 2022 watapata msamaha wa tozo kwa kiwango cha asilimia 50

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na watendaji wa kiwanda cha sukari Kagera alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Kanali Wilson Sakulo.

“Niwaombe sana wawekezaji wote, waajiri wote nendeni mkashirikiane na NSSF kwenye ofa hii ambayo katika Mfuko tumeweza kupata msamaha huu hivyo tuitumie vizuri nafasi hii,” amesema.

Mwekezaji wa kiwanda cha sukari cha Kagera, Seif Seif akimuonesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kulia), namna wanavyotumia maji kutoka Mto Kagera kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji wa miwa katika kiwanda hicho, wakati wa ziara ya Waziri Jenista katika kiwanda hicho.

Ameishukuru NSSF kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama na wadau ili kuhakikisha wanapata huduma nzuri, ambapo alitoa wito kwa waajiri wengine wote waliopo kwenye sekta binafsi kuhakikisha wanajisajili na kuwasajili wafanyakazi wao pamoja na kuwapelekea michango yao NSSF kwa wakati kwani hilo ni takwa la kisheria.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora aliupongeza Mfuko wa NSSF katika mkoa huo kwa kuweza kupunguza kero za wanachama na wadau kwa asilimia zaidi ya 90 kutokana na muda mrefu sasa uongozi wa mkoa huo haujapokea malalamiko yoyote ya wanachama wa NSSF.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, enista Mhagama, akipata maelezo kuhusu mradi wa shamba la miwa Kagera kutoka kwa Mhandisi Francisco Sikalumbi wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha sukari Kagera. Kushoto ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cosmas Sasi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba, amesema kiwanda cha sukari cha Kagera kwa upande wa NSSF ni mdau mkubwa kwani kina wanachama 8,000 ambao wanachangia kila mwezi takribani Shilingi milioni 540.

Aidha, mbunge wa Nkenge, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Florent Kyambo, amesema mwekezaji huyo licha ya kutengeneza ajira kwa Watanzania, lakini ni mlipaji mzuri wa michango ya wafanyakazi wake NSSF.

Naye, mwekezaji wa kiwanda cha sukari Kagera, Seif Seif amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwa na dira ya kukuza viwanda vya ndani na kuweza kuvilinda ili viweze kukua.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wahandisi wa kilimo wanaofanyakazi katika kiwanda cha sukari Kagera, alipotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Kulia ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif na kushoto ni Mbunge wa Nkenge, Florent Kyambo

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Mhandisi Atugonza Phinis ambaye ni mwendeshaji mitambo kiwandani hapo, amesema kampuni ya Kagera imekuwa ikitoa ajira nyingi kwa vijana na kwamba wanafurahishwa na namna mwekezaji huyo anavyojali maslahi ya wafanyakazi wake kwa kuwasilisha michango NSSF ili pale watakapopatwa na janga waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko huo.