April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Mameneja wa Hoteli zilizopata nyota za ubora daraja la kwanza katika hafla ya Ugawaji madaraja ya nyota kwa Hoteli za Jijini Dodoma, Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda akiwa na Makatibu Wakuu wa wizara nyingine walioalikwa katika hafla hiyo, Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Aloyce Nzuki. [ Picha zote na Wizara ya Maliasili na Utalii)

Serikali yakaribisha wawekezaji kujenga hoteli za nyota 4, 5 Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imewataka wawekezaji nchini kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Hoteli zenye nyota 4 ama 5 kutokana na kutokuwepo katika Jiji la Dodoma baada ya serikali kutangaza hoteli 3 pekee ndizo zenye nyota tatu za Jijini Dodoma ambazo ni Fantacy Village, Nashera Hoteli na New Dodoma Hotel.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akimkabidhi tuzo ya hadhi ya nyota tatu Meneja wa Hoteli ya Fantasy Village Omary Birango katika hafla iliyofanyika leo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu akimkabidi Nyota tatu (3) kwa Kaimu Meneja wa Nashera Hotel Ms. Epiphania Ponera kwenye halfa ya utoaji Nyota kwa hoteli zilizokidhi vigezo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Veta jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu katika hafla ya kutoa Daraja za Nyota kwa hoteli zilizopangwa katika daraja za ubora za jijini Dodoma.

Kanyasu amesema licha ya Jiji la Dodoma kuwa ndio Makao Makuu ya Serikali lakini bado kuna mahitaji ya hoteli zenye nyota 4 na 5 hivyo amewataka wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga hoteli zenye ubora.

“Wito wangu hatuna hoteli zenye nyota 4 na 5 hapa Dodoma, niwaombe wawekezaji kuchangamkia fursa hii, kutafuta maeneo kwani Jiji la Dodoma linatoa na maeneo hayo yapo,”amesema.

Amesema uwepo wa hoteli nzuri kutachangia kuwafanya watalii ambao huja nchini kufikia katika maeneo yenye ubora hivyo kuliongezea taifa mapato.

“Hitaji la wageni ni malazi na huduma bora hivyo upangaji wa madaraja ni jambo muhimu ,wito wangu kwa wamiliki wa hoteli kuwa na lugha nzuri kwa wageni ambao wanawapokea,” amesema.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akimkabidhi tuzo ya hadhi ya nyota mbili Meneja wa Hoteli ya Morena, Edwin Leyla katika hafla iliyofanyika leo Jijini Dodoma.

Kanyasu pia amesema changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo ni hoteli kujengwa sehemu ambazo sio sahihi pamoja na kuwepo kwa wafanyakazi wasio na sifa.

“Niwaombe wamiliki wa hoteli ambazo tumezikagua na kukuta hazijakidhi vigezo kuliangalia kwa umakini jambo hili kwa kujenga sehemu sahihi pamoja na kuchagua wafanyakazi wenye sifa,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda akizungumza kwenye hafla ya utoaji Nyota kwenye hoteli zilizokidhi vigezo iliyofanyika leo Jijini Dodoma

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda amesema zoezi la kupanga madaraja ya nyota kwa hoteli lilianza katika Mikoa ya Dar es salaa, Pwani, Arusha, Mara na sasa Dodoma.

Amesema lengo la zoezi hilo ni kubaini ubora wa hoteli ili kuwasaidia Watanzania pamoja na wageni ambao wanatoka nje ya Tanzania kujua ni sehemu gani wanatakiwa kufikia pindi wanapokuja nchini na kujua ubora wa hoteli.

Amesema wameanzisha mfumo wa kieletroniki ambao utakuwa ukiwawezesha wamiliki wa hoteli kupima ubora wa hoteli zao. Mkenda amesema kwa Jiji la Dodoma walikagua, hoteli, nyumba za wageni 428 ambapo walizokuta zenye ubora ni 24 pekee.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa na baadhi ya viongozi na watumishi wa Idara ya Utalii kwenye picha ya pamoja leo katika hafla ya utoaji nyota katika Hoteli zilizokidhi vigezo jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii leo katika hafla ya utoaji nyota katika Hoteli zilizokidhi vigezo vya ubora iliyofanyika jijini Dodoma.

Naye, Mtaalamu watathmini wa Ubora wa Hoteli,Hassan Rehani amesema wamekuwa wakitoa  nyota za hoteli kutokana na kujaza madodoso ambayo baadae huangalia ubora,pamoja na kutumia vigezo tisa ikiwemo kuwepo kwa vifaa vya kuzuia majanga.

 “Changamoto ambazo tumekuwa tukikutana nazo kwanza ni kutokupewa ushirikiano kutokana na wengi kujua sisi ni askari,wafanyakazi kuwa na uwezo mdogo pamoja na kutokuwepo kwa wahusika pindi wanapokuwa wakiwahitaji,” amesema.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Mameneja wa Hoteli zilizopata nyota za ubora daraja la kwanza katika hafla ya Ugawaji madaraja ya nyota kwa Hoteli za Jijini Dodoma, Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda akiwa na Makatibu Wakuu wa wizara nyingine walioalikwa katika hafla hiyo, Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Aloyce Nzuki.
( Picha zote na Wizara ya Maliasili na Utalii)