October 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufugaji samaki wafungua fursa kwa vijana

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

UFUGAJI wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria umefungua fursa za ajira na kujipatia kipato kwa vijana na wananchi wengine, huku ukichochea ukuaji wa biashara zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa uvuvi.

Fursa hiyo imeanza kuzaa matunda kwa kikundi cha Kitwima Youth Group kilichopo mtaa wa Kisoko, Kata ya Luchelele wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, ambacho kimeanza kuvuna samaki baada ya kupata mkopo wa sh.milioni 106.9 kupitia Programu ya sh.bilioni 200 ya kuwawezesha vijana.

Akizungumza katika hafla ya uvunaji iliyofanyika Oktoba 25, 2026, katika mtaa wa Kisoko Kata ya Lechelele jijini Mwanza,Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana  Dkt. Kedmon Mapana kwa niaba ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana Dkt.Joel Nanauka amesema,mafanikio ya vijana hao yanaonesha kuwa Serikali inaweza kuwawezesha vijana wanaoungana na kuandaa miradi yenye tija badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa.

Amesema,Kikundi hicho chenye wanachama saba kilipatiwa mkopo Machi 10, 2026, na kinatarajia kuvuna takribani tani 15 za samaki kutoka katika vizimba sita, zitakazouzwa kwa zaidi ya sh.milioni 127 wakati walipatiwa mkopo wa sh.milioni 106.9,hivyo ndani ya kipindi kifupi cha miezi sita wamepata faida.Kama Wizara wanategemea watoke kwenye vizimba  sita na mwakani wawe na vizimba 8,10,12,20 wanaendelea hivyo hivyo.

“Kushuhudia matokeo haya ya leo ni ujumbe tosha kwa vijana wengine hapa nchini, kama kweli mnania ya dhati ya kuunda vikundi vidogo vidogo, Serikali inaweza kuwawezesha na wasikalie kulalamika na kuandamana,”amesema Dkt.Mapana.

Dkt.Mapana amewapongeza vijana hao kwa mipango yao ya kurejesha mkopo kwa wakati, akiwataka kuongeza vizimba na kuendeleza mradi. Pia amewahimiza vijana kujisajili katika mfumo wa YES kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ili kupata taarifa za fursa zinazotolewa na Serikali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbemaji Maji Baridi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Yohana Mirumbe, amesema mafanikio hayo yanaonesha nafasi ya uchumi wa buluu katika kubadili maisha ya vijana na kuchangia maendeleo ya Taifa huku mnyororo wa thamani wa ufugaji samaki una fursa nyingi, zikiwemo uzalishaji wa vifaranga, utengenezaji wa vizimba, uzalishaji wa chakula cha samaki, uvunaji, usafirishaji, usindikaji na masoko.

Naye Mkuu wa Biashara Changa na Uwezeshaji wa CRDB Bank Foundation, Fadhil Bushagama amesema,wamekuwa wakitoa elimu ya  fedha na wamefarijika kuona mtaji uliotolewa kwa vijana hao ukitumika kwa malengo yaliyokusudiwa hadi kufikia hatua ya mavuno.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa uwezeshaji unaweza kuongeza ajira na kipato, huku akiwataka vijana wengine kutumia fursa zilizopo na kuzingatia uaminifu katika kusimamia mitaji wanayopewa.

Mwenyekiti wa kikundi cha  Kitwima Youth Group, Suzana Sayi amesema, kikundi hicho chenye wanawake watatu na wanaume wanne kimejipanga kupanua mradi na kufikia vizimba 10 hadi 100  ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wanachama.

Amesema mipango mingine ni kununua boti yenye injini, kujenga ghala la kuhifadhia chakula cha samaki na kuimarisha usalama wa eneo la mradi ili kuongeza ufanisi wa shughuli za ufugaji.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, mkazi wa Luchelele, Seif Damian amesema,wananchi wa maeneo hayo  sasa wanapata samaki kwa urahisi, huku vijana wakipata fursa za kujipatia kipato kupitia usafirishaji wa wanunuzi kwa bodaboda na bajaji,pia vijana wamepata nafasi za kazi za kulisha samaki katika vizimba, hatua inayochangia kuongeza mzunguko wa fedha na shughuli za biashara katika eneo hilo.

Awali akisoma  taarifa ya utekelezaji wa mradi huo  Katibu  wa kikundi cha Kitwima Youth Group wake, Bung’e Nawe Kwaangw amesema,kikundi kilipandikiza vifaranga 66,000 katika vizimba sita Machi 17, 2026,huku lengo la kikundi hicho ni kuongeza uzalishaji wa samaki nchini Tanzania na kupunguza pengo la upatikanaji wa samaki kupitia ufugaji endelevu wa sato.

 Pia kuwa shamba darasa la mfano kwa vijana na wafugaji wengine, pamoja na kujijengea hadhi ya kuwa Kitovu cha Ubora katika ufugaji wa kisasa wa samaki nchini Tanzania,kupitia mafunzo ya vitendo, ubunifu, teknolojia na usimamizi bora wa uzalishaji, shamba litakuwa sehemu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuendeleza mbinu endelevu za ufugaji wa samaki.

Vilevile kuboresha ufanisi wa matumizi ya chakula cha samaki  ili kupunguza upotevu wa chakula, kushusha gharama za uzalishaji na kuongeza faida,kufikia mfumo wa uzalishaji usiozalisha taka kwa njia bunifu, ikiwemo usindikaji na uongezaji thamani wa bidhaa za samaki.

Naye Ofisa Maendeleo ya Vijana Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Diana Francis, amewataka vijana kutumia majukwaa ya vijana kupata taarifa kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.

0-3840×1742-0-0#
0-3840×1742-0-0#
0-3840×1742-0-0#