September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TanTrade yafungua soko Afrika Mashariki 

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza 

IMEELEKEZWA kuwa mikoa sita ya Kanda ya Ziwa imechangia kiasi cha sh. trilioni 54.4, sawa na asilimia 23 ya Pato la Taifa kwa mwaka jana, huku Mkoa wa Mwanza pekee ukichangia sh.trilioni 14.7, sawa na asilimia 7.2 ya Pato la Taifa.

Hayo yameelezwa Septemba 3,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la mamlaka  hiyo katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela jijini Mwanza yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la mamlaka  hiyo katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela jijini Mwanza.

Ambapo Mafuru amesema,takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa Kanda ya Ziwa katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na mchango wake katika Pato la Taifa, hivyo  Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki kuwa muhimu kufanyika jijini Mwanza na yamekuwa kiungo kikubwa cha kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki lenye wakazi milioni 507.

Mafuru amesema,soko hilo linatoa fursa kwa wazalishaji,wafanyabiashara na wasambazaji wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania, huku zaidi ya waoneshaji 250 wakishiriki katika maonesho hayo.

Pia amesema,TanTrade inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na kwamba kazi ya mamlaka hiyo si Maonesho ya Sabasaba pekee jijini Dar-es-Salaam, bali ni ndani na nje ya nchi, huku katika maonesho hayo wakikutana na wateja wengi kutoka katika Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki.

Huku akisitiza kuwa TanTrade inasikia fahari kushirikiana na wafanyabiashara, hasa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, ambayo imefanya kazi kubwa na kuwezesha kupatikana kwa wazalishaji wanaoshiriki katika maonesho hayo.

Amesema kazi ya TanTrade katika kuratibu maonesho hayo ni kuwawezesha wafanyabiashara kuingia katika soko la Afrika Mashariki lenye wakazi milioni 507, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na nembo ya “Made in Tanzania” inayothibitisha ubora na uhalisia wa bidhaa.

Hata hivyo amesema,bidhaa zinazothibitishwa na taasisi kama TBS zinapaswa kuwa na ubora na uzito wa kutosha, akieleza kuwa taasisi hizo zinaaminika kimataifa na kwamba uthibitisho wa TBS unatambulika Tanzania, Afrika Mashariki na Jumuiya ya Afrika.

Amesema Watanzania wanapaswa kuunga mkono juhudi za Rais za kufanya mapinduzi katika sekta ya biashara ili mchango wa sekta hiyo uendelee kuongezeka katika uchumi wa nchi na mapinduzi hayo yaingie mfukoni mwa Watanzania.

“Tusiziimbe fursa pekee yake. Tuna maziwa makubwa, tuna ardhi, tuna mito; je, umefanya nini? Fanya kazi, ongeza kipato chako mmoja mmoja na Taifa,” amesema.

Mafuru amesema hakuna haja ya kuongelea fursa pekee yake bila kuzalisha kwa ubora, kuongeza thamani na kufikia masoko yanayoweza kutoa faida, akieleza kuwa Kanda ya Ziwa inaongoza katika uzalishaji wa dhahabu ikiwemo  Geita,lakini baadhi ya maeneo yanaendelea kutumia bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.

Akitolea mfano  Katoro, asilimia 90 ya bidhaa zinazotumika, ukiondoa chakula, zinatoka nje, hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo Watanzania wanaozalisha bidhaa wazalishe kwa wingi ili washindane kimataifa, huku taasisi za Serikali zikibadili mtazamo kutoka kuwa wadhibiti na kuwa wawezeshaji.

Msimamizi Mkuu wa ofisi ya TanTrade Kanda ya Ziwa Cecilia Mwandepa (kulia),akimsikiliza mwananchi (kushoto), aliyetembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela jijini Mwanza yaliyoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake,Meneja wa Huduma kwa Wateja wa kampuni ya Proofings kutoka nchini Uganda, Kigozi Henry,ambayo imekuwa mahindi wa jumla katika maonesho hayo  amesema, wamekuwa wakishiriki kila mwaka na kutengeneza bidhaa za ujenzi huku akipongeza ushirikiano kati ya TanTrade na TCCIA uliowapa fursa ya kuonesha bidhaa zao kwa Watanzania.

Naye mjasiriamali aliyeshiriki katika maonesho hayo,Mercy Ntabago, ametoa wito kwa wakulima wanaolima na kuzalisha bidhaa asilia  kujitokeza kutumia fursa zinazotolewa na TanTrade, akisema mamlaka hiyo inawapa elimu, masoko mazuri na kuwavusha nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuweka nembo ya “Made in Tanzania” kwenye bidhaa zao.