April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yachukua hatua mbalimbali kupambana na Covid-19

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

IMEELEZWA kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupambana na Covid-19,ikiwemo kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya kama vile ya kusimika mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni pamoja na utoaji wa chanjo dhidi ya janga hilo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,Dkt. Leonard Subi,wakati akifungua mkutano wa kimtandao wa elimu juu ya umuhimu wa utoaji chanjo ya COvid-19 nchini hapa kwa waandishi wa habari na Azaki, ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza(MPC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Freedom House.

Dkt.Subi amesema,wameimarisha miundombinu ya utoaji huduma za afya katika hospitali ikiwemo hupatikanaji wa hewa tiba ya oksijeni.

Amesema,awali suala la oksijeni nalo lilikuwa changamoto lakini katika mlipuko huo wameendelea kuimarisha miundombinu hiyo.

“Serikali hii ya awamu ya sita tumesimika mitambo mipya saba ya uzalishaji wa hewa ya oksijeni katika hospitali saba za rufaa za mikoa,na kila mtambo unaweza kuzalisha mitungi 200 ya oksijeni kwa siku na kwa wakati,”amesema Dkt.Subi.

Pia amesema,wanaendelea hivi sasa na usindikaji wa mitambo mingine 12 katika hospitali zao za rufaa za mikoa na katika mitambo hiyo serikali imetoa zaidi ya bilioni 10 kwa ajili ya kuhakikisha wanaimarisha huduma kwa wananchi.

Aidha amesema,wataendelea na usimikaji wa mitambo ya oksijeni na wapo katika mpango wa usimikaji mitambo ya oksijeni 25, katika hospitali za rufaa za mikoa,baadhi za wilaya na za Kanda,lengo ni kuwa hata baada ya COvid-19 wawe na miundombinu madhubuti ya kuwezesha hupatikanaji wa hewa ya oksijeni,kwa wananchi.

Sanjari na hayo amesema,Julai 28,walianza kutoa chanjo ambapo ilizinduliwa na Rais na kisha kuanza kusambaza mikoa yote Tanzania Bara hivyo wakati wanaanza utoaji chanjo katika mikoa Agosti 3 mwaka 2021.

Walianza na vituo vya kutolea chanjo 550 lakini sasa wametanua wigo na Sasa Wana vituo zaidi ya 1548 na watazidi kutanua ili kuhakikisha vituo vyote vinavotoa chanjo vinawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini na wao wanapata huduma hizo za chanjo.

“Tumeanza kutoa chanjo ambayo ni hatua kubwa kwani ni moja ya kinga inayoaminika duniani,na ilianza kutolewa siku nyingi miaka mingi tumeona magonjwa kama ya ndui,polio yamepotea kabisa,pepo punda hususani kwa watoto wachanga yameendelea kutokomea,tutaendelea kuhamasisha watanzania kujumuika na serikali yao katika mapambano dhidi ya COvid-19 na kuhamasisha wananchi kupata chanjo ambayo ni hiari,”amesema Dkt.Subi.

Akizungumzia umuhimu wa chanjo ya Covid 19,Daktari Bingwa Mwandamizi wa magonjwa ya ndani na moyo kutoka (JKCI),Profesa Harun Nyagori,amesema chanjo ya COvid-19 ni salama na haina madhara yoyote kwenye mifumo ya uzazi wala haisababishi kuganda kwa damu kama inavyoelezwa.

Mkurugenzi wa shirika la Freedom House,Daniel Lema ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutoa wataalamu ambao wameweza kutoa majibu ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa na jamii juu ya chanjo ya COvid-19.

Lema amewaomba wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kutoruhusu uvumi wa taarifa zisizo na ukweli kupata nguvu kutoka kwa watu ambao wana lengo baya la kupotosha ukweli uliopo.