Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Madini ameielekeza Tume ya Madini kutotangaza bei elekezi ya makaa ya mawe bila kushirikisha wadau wa sekta hiyo.
Mavunde amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha bei hizo zinaendana na uhalisia wa soko la dunia na kulinda maslahi ya wachimbaji, wasafirishaji pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao na wadau wa sekta ya makaa ya mawe kilichowakutanisha wachimbaji wakubwa na wadogo, wafanyabiashara na wasafirishaji,Mavunde alisistiza umuhimu wa kuwashirikisha wadau katika mchakato wa upangaji wa bei elekezi ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na maamuzi yasiyojumuisha maoni yao.
Aidha amewahimiza wadau kuanzisha umoja wao utakaosaidia kuwasilisha kwa pamoja maslahi yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta hiyo.
Awali, wadau hao, wakiwemo viongozi wa juu wa baadhi ya makampuni ya makaa ya mawe nchini, walieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika sekta hiyo.
Walisema,miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na bei elekezi zisizoendana na hali halisi ya soko, makato ya mrabaha, pamoja na uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaounda makundi ya kupanga bei kwa pamoja kinyume na sheria.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Sundi Malomo, alitumia fursa hiyo kueleza taratibu zinazotumika katika upangaji wa bei za madini, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia miongozo iliyopo ili kuhakikisha uwazi na usawa katika sekta hiyo.
Aidha amesema ,mara nyingi vinapoitishwa vikao vya kupanga bei ya makaa ya mawe,wadau wengi huwa hawajitokezi na matokeo yake wadau wachache wanaokuwepo ndio hupanga bei hiyo.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT