May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe wa kwanza (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa kiwanda cha Bugiri Investment Bw.Nkuba Bugiri alipokuwa anamueleza mambo mbalimbali kuhusu kiwanda hicho. Wa kwanza (kushoto) ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Ludovick Nduhiye.

Serikali: Viwanda vitumia malighafi za ndani

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe amewataka Watanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.

Sehemu ya shehena ya mbegu za alizeti zilizopo kiwandani hapo zikiwa tayari kwa ajili ya uzalishaji

Prof. Shemdoe ameyasema hayo nkoani Simiyu alipokuwa katika ziara ya siku moja kutembelea viwanda katika Mkoa huo. Katika ziara hiyo Katibu Mkuu na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea kiwanda kipya cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha cha Bugari Investment Ltd kinachomilikiwa na Mtanzania kwa asilimia 100.

Prof Shemdoe amesema Bugari ameonesha umuhimu wa kuwa na malengo katika kutekeleza jambo lolote.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe wa kwanza (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa kiwanda cha Bugiri Investment Bw.Nkuba Bugiri alipokuwa anamueleza mambo mbalimbali kuhusu kiwanda hicho. Wa kwanza (kushoto) ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Ludovick Nduhiye.

“Ukiwa na malengo unaweza kufanya kitu chochote, hivyo natoa rai kwa watanzania wengine ambao wanaweza kuiga mfano huu kufika mahali hapa na kujifunza, maana yote yanawezekana ukiweka nia,”amesema.

Kiwanda cha Bugari Investment Ltd kimejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 2 kinatarajiwa kutoa ajira kwa Watanzania 65 ikiwa ni ajira za kudumu na za muda pamoja na kuchangia mapato kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali.

Prof Shemdoe ameishukuru Serikali ya mkoa kwa kumpa ushirikiano mwekezaji huyo na kumuwezesha kufanikisha kutimiza azma yake ya kujenga kiwanda. Pia alizishukuru Taasisi za fedha kwa kumuamini na kumpatia mkopo uliofanikisha kujenga kiwanda hicho.

Sehemu ya mashine za kukamulia mafuta ya alizeti katika kiwanda cha Bugiri Investment kilichopo Wilaya ya Maswa Mkoa wa Shinyanga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga amesema wananchi wa Simiyu na mikoa ya jirani wamepata uhakika wa soko la alizeti kwa kuwepo kiwanda hicho.

“Tumekuwa tukiwasisitiza wananchi kulima, lakini changamoto iilikuwa upatikanaji wa masoko, hivyo uwepo wa kiwanda hiki utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa huu na mikoa jirani’’.

Aidha ametoa wito kwa wananchi wa bariadi kuendelea kuzalisha alizeti kwa wingi ili kiwanda kiendelee kupata malighafi ya kutosha.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda hicho, Nkuba Bugari amesema ujenzi wa kiwanda hicho umeanza mwaka 2015 na upo katika hatua za mwisho na ujenzi na kinatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji mapema hivi karibuni.

Bugari amesema wazo la kujenga kiwanda hicho alipata baada ya kupata hamasa kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli alipotoa rai kwa Watanzania kujenga viwanda.

“Ndugu Watanzania wezangu tusiache bahati hii ya kuwa na Magufuli, ni kwa namna gani, Rais anajitoa kwa ajili Watanzania katika kufanikisha Tanzania ya Viwanda,”amesema.

Sehemu ya mashine za kukamulia mafuta ya alizeti katika kiwanda cha Bugiri Investment kilichopo Wilaya ya Maswa Mkoa wa Shinyanga.

Amesema mashine zilizofungwa katika kiwanda hicho zina uwezo wa kuchakata mbegu za alizeti, pamba na karanga.

Ameongeza kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani elfu arobaini na nane za mbegu za alizeti. Hivyo lengo lao ni kushika soko la ndani pamoja kuuza mafuta hayo nje ya nchi ya Tanzania.Aidha aliwasisitiza watanzania kuwa na uthubutu katika kutimiza malengo mbalimbali.