January 19, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwekeza zaidi utafiti zao la kahawa na kutoa elimu

Na Martha Fatael, TimesMajira,Online Moshi

SERIKALI imetangaza kuwekeza zaidi kwenye utafiti wa zao la kahawa pamoja na kutoa elimu kwa maofisa ugani ili kusaidia ufufuaji na kuanzishwa mashamba mapya yenye tija kwa kilimo cha zao hilo nchini.

Aidha Serikali imeongeza bajeti ya huduma ugani kutoka sh. milioni 600 kwa mwaka hadi sh. bilioni 11.5 kwa kipindi hicho kama njia kuu ya kusaidia jitihada za kitaifa kufufua sekta ya Kilimo Nchini.

Waziri wa Kilimo, Prof Adolph Mkenda amesema hayo wakati akizindua maonesho ya kitaifa ya Kahawa yaliyopewa jina la ‘Kahawa Festival’ yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru Park katika Manispaa ya Moshi kuanzia Oktoba 1, mwaka huu yakitarajiwa kumalizika leo.

Hata hivyo, Serikali imesema imehakikishiwa na Benki za NMB, Azania, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) kuwa zipo tayari kukopesha wakulima wabadilim iche ya kahawa kutoka ya zamani hadi mpya ili kuongeza tija ya zao Hilo.

Utafiti unaonesha kuwa ipo baadhi ya mikoa nchini inaendeleza kilimo cha kahawa kwa kutumia miche ya zamani ambayo ina wastani wa miaka 20 hadi 40 na hivyo kuwa na uzalishaji mdogo usiomudu ushindani katika soko.

Amesema benki hizo zimeahidi kuwasaidia wakulima ili kupata fedha za kubadili mibuni ya zamani huku akitaka vijana kujikita katika Kilimo hicho badala ya mfumo wa sasa kuwaacha wazee pekee.

Kadhalika waziri Mkenda amewataka wakulima kutumia mbegu zinazomudu visumbufu vya zao Hilo kutoka Taasisi ya utafiti wa Kahawa Nchini (TaCRI) na kutaka bodi ya Kahawa Nchini (TCB) kuratibu mchakato huo.

Prof Mkenda amesema pamoja na changamoto zinazoonekana katika zao Hilo yapo mafanikio yameanza kuonekana ambapo kupitia utafiti wa TaCRI baadhi ya mashamba Uzalishaji umepanda kutoka Kilo 250 kwa hekta Moja hadi kilo 600 kwa Hekta hiyo hiyo.

Mapema mratibu wa mradi wa kuongeza thamani ya bidhaa za mazao, (MARKUP), Tawi la Tanzania, Msafiri Fungo amesema zaidi ya wajasiriamali 300 pamoja na Taasisi 21 nchini zikiwamo za umma na binafsi zimenufaika miamala yenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani sh. milioni 1.5

Amesema mradi kupitia MARKUP umejikita kusaidia wajasiriamali na Taasisi za Kilimo kutafuta masoko na kuvutia mitaji kutoka nje ili kuvutia uwekezaji, lakini pia kusaidia nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza matakwa ya mikataba na itifaki Jumuiya ya Afrika Mashariki.