December 6, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yawahakikishia mikopo nafuu endelevu wakulima, wavuvi na wafugaji

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imewahakikishia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa itawapa mikopo yenye riba nafuu bila kuchoka ili kuchochea uzalishaji wa mazao sambamba kuimarisha minyororo wa thamani katika sekta hizo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Kimataifa ya Huduma katika makao makuu ya benki hiyo, Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji wa TADB, Derick Lugemala, alisema benki hiyo inatambua mchango wa wadau katika mnyororo mzima wa thamani na kwa hiyo inawajibu wa kuwaunga mkono kwa kuwapa mikopo wanayoimudu ili kukuza uzalishaji.

“Sisi kama benki ya maendeleo ya kilimo hatufanyi kazi na mteja bali tunamuangalia mteja wetu kama mradi. Kwa sababu hiyo ni lazima tumuelewe mteja, tuelewe biashara anayofanya, wapi anaponunua malighafi na namna anavyochakata mazao hayo.

Lengo ni kuongeza thamani na kuleta tija katika uzalishaji,” alisema Lugemala.

Amesema kuwa benki imekuwa ikitekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 na kwamba mikopo ambayo benki imekuwa ikitoa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi lengo lake limekuwa ni kutoa msukumo stahiki katika ujenzi wa viwanda.

Mkurugenzi wa fedha na uwekezaji wa Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB), Derick Lugemala, akizungumza na wateja na wafanyakazi wa benki hiyo wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo Jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Hadi Juni, mwaka huu benki ilikuwa imetoa kwa sekta ya kilimo pekee jumla ya sh. 429,000,868,790.58 Kati ya fedha hizo, kwa mfano, 246,488,453,466.38 zilielekezwa katika kuendeleza minyororo ya thamani, 15,127,722,059.21 walipewa waombaji kununua mitambo ya kilimo na 141,495,930,116.19 walipewa wazalishaji wanaofanya biashara.

Lugemala ameeleza kuwa moja ya malengo ya benki hiyo ni kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuhakikisha wakulima wadogo wanapatiwa mikopo na elimu juu ya kuongeza tija katika uzalishaji na thamani ya mazao.

“Sisi kama benki ya wakulima kazi yetu kubwa hasa ni kumuinua mkulima kiuchumi kwa kumpatia mkopo wenye riba nafuu sambamba na kumpa elimu juu ya kuongeza tija katika uzalishaji na thamani ya mazao anayozalisha,’’ amesema na kuongeza kuwa

Amesema wiki hii itaiwezesha benki kutambua mafanikio na changamoto wanazokutana nazo wateja wao na kuona namna ya kuwafikia watu wengi zaidi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tobi Peanut Butter, Agatha Laizer, wasindikaji wa karanga na korosho, ameipongeza TADB kwa kuwajali wateja na kwamba benki hiyo imefanikisha ndoto zao kwa kuwapa mikopo sambamba na kuwapa elimu elimu ya kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha.

“Naipongeza Benki ya TADB kwani imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa wajasiriamali wadogo kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu ambayo imekuwa ikituinua kiuchumi na kuongeza ajira. Bila mikopo yao tungekwama,” amesema Bi. Laizer.

Lengidu Abdallah ambaye ni mfugaji ameishukuru Benki kwa kuwapa mkopo ambao umewasaidia kununua chakula cha ngo’mbe na kununua mbegu bora ya ngo’mbe na kuahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na benki hiyo .

“Napenda kuishukuru TADB kwa mkopo ambao umetuwezesha kupata chakula cha ngo’mbe na kununua mbegu bora ya ngo’mbe. Tutabaki karibu na benki hii,” ameeleza, Abdallah.

Wiki ya Huduma kwa wateja huadhimishwa kila mwaka katika wiki ya mwanzo ya mwezi Oktoba kote duniani. TABD huadhimisha wiki hii ili kutoa nafasi kwa wateja na wadau wengine kujifunza na kuzijua huduma na bidhaa za benki hiyo.