May 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usimikaji mitambo hewa tiba wamkosha Kihongosi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Moshi

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan, kutoa zaidi ya Sh.Bil 1.9 katika mradi wa ujenzi wa kimkakati wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) ni mzuri kwani unaokoa maisha ya watanzania.

Aidha, amesema mradi huo ambao unapunguza gharama za uendeshaji, utatumika kutoa huduma katika maeneo mengine ambayo yana upungufu au uhitaji wa hewa tiba.

Akizungumza leo Mei 30,2026 katika hospitali hiyo alipokwenda kutembelea na kukagua mradi huo wa ‘Oxgen Plant’, Kihongosi amesema kabla ya uwekezaji huo kulikuwa na changamoto nyingi, ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji na upatikanaji wa hewa tiba kwani ilikuwa hadi iagizwe nje ya mkoa, Dar es Salaam au Arusha na maeneo mengine, jambo ambalo lilikuwa linaongeza gharama kubwa za uendeshaji wa hospitali.

“Kazi ya utabibu inahitaji moyo wa upendo kuhudumia wagonjwa, kwa kuwa sio kila mtu anaweza akaifanya kazi hiyo, kwa vile ni kazi ya wito mkubwa. Niwaombe tuilinde miundombinu hii,”amesema Kihongosi.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, Dk. Abdillah Bakari, akitoa taarifa ya miradi inayotekelezwa, amesema kwa wiki moja hospitali hiyo ilikuwa ikitumia mitungi 100 mpaka 110.

Kutokana na mahitaji kuongezeka, inakadiriwa kwa hali ya kawaida mitungi itaongezeka hadi kufikia mitungi 150 kipindi cha uhitaji mkubwa.”Taasisi ilikuwa ikitumia kiasi cha sh. 3,500,000 kwa wiki, kwa ajili ya manunuzi ya hewa tiba ya oksijeni. Hospitali ilikuwa inatenga bajeti ya Sh.Mil 100 hadi 200 kwa mwaka, kwa ajili ya manunuzi ya hewa tiba ya oksijeni,”amesema Dk. Bakari.

Kwa mujibu wa Dk. Bakari, hospitali ya Rufani ya Mawenzi inahudumia wagonjwa wa nje 322 mpaka 500 wastani kwa siku.Huku ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 450.

Kutokana na uhitaji huo, Dk. Abdillah, amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia (Global Fund), iliamua kusimika mtambo wa kuzalisha hewa tiba (oksijeni) ndani ya hospitali.

Zaidi alifafanua,”Hatua hii ililenga kuhakikisha upatikanaji wa hewa tiba ya oksijeni kwa uhakika, kupunguza gharama za kununua kutoka nje, na kuimarisha huduma za dharura kwa wagonjwa mahututi, wamama wajawazito, watoto wachanga, na wagonjwa wenye changamoto za mfumo wa hewa,”ameeleza.

Amesisitiza, kupatikana kwa hewa tiba ya oksijeni ya uhakika kumesaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuongeza imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na hospitali ya MawenThamani ya mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, ni dola za Marekani 843,217,04 sawa na zaidi ya Sh. bilioni 1.940 ikijumuisha gharama za mitambo, ujenzi wa jengo, jenereta na gharama za usimikaji.