Na Mwandishi Wetu, Handeni
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Salum Nyamwese amesema ujio wa Shirika la World Vision kwenye Tarafa ya Mkumburu ni kwenda kuwakomboa wananchi kwenye kupata huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji, lishe, maendeleo ya watoto na ustawi wa jamii.
Ameyasema hayo Mei 28, 2026 kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya miradi iliyotekelezwa na Shirika la World Vision, Mkumburu AP iliyofanyika Kijiji cha Masatu, Kata ya Segera, na kuongeza kuwa kwa kwa mchango huo inalotoa shirika hilo, linaisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa Taifa la Tanzania.

“Viongozi na wananchi na nyie mmekuwa mashuhuda, World Vision yupo hapa Mkumburu tangu mwaka 2013, mpaka leo amekuwa ni mdau mkubwa katika kutuletea wananchi maendeleo. Na mpango wao mkubwa umekuwa kwenye kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya elimu, afya, maji, lishe, maendeleo ya watoto, ustawi wa jamii, pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi kwa kaya mbalimbali” amesema Nyamwese.
Nyamwese amesema wamekwenda kwenye hafla hiyo sio tu kwa ajili ya kukabidhiwa matenki ya maji na vyoo vilivyojengwa kwa ufadhili wa Shirika la World Vision, bali ni kuona ushirikiano uliopo kati ya Serikali na wadau wa maendeleo wakiwemo Shirika la World, na wananchi wanatakiwa wajifunze kuwa wana uwezo wa kumaliza changamoto ndogo ndogo zinapotokea ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo.
Nyamwese amesema miradi inapojengwa na Shirika la World na kuikamilisha inakuwa sio ya kwao tena, bali ya wananchi, hivyo wanapaswa kuilinda iwe endelevu, kwani miradi hiyo iliibuliwa na wananchi wenyewe, na shirika hilo likawa watekelezaji katika kujenga miradi hiyo, hivyo inapoharibika mikononi mwao wananchi, itaonesha hawakuhitaji miradi hiyo.
“Miradi hii ya matenki ipo nane (8) kwenye shule nane. Hivyo, nitoe wito kupitia mradi huu, nataka miradi yote minane (8) tuilinde. Miradi hii ipo kwetu, hivyo tuilinde, tuithamini. Inatakiwa ilindwe na wananchi wenyewe ili iwe endelevu, na inapotokea kuharibika uongozi wa Halmashauri ya Wilaya na wananchi wanatakiwa kuifanyia ukarabati” amesema Nyamwese.

Mwakilishi wa Meneja wa Shirika la World Vision Kanda ya Kaskazini, Malombe Chalo, amesena wanaishukuru Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, viongozi ngazi ya kata na vijiji pamoja na wananchi, kwani wameweza kutoa ushirikiano wa kutosha, na wakawezesha wao kuweza kuwahudumia wananchi.
Naye Diwani wa Kata ya Segera, Onesmo Makomelo, amesema Shirika la World Vision ni mkombozi kwa Kijiji cha Masatu, kwani Shule ya Msingi ya Kijiji hicho ilijengwa tangu mwaka 1963, hivyo kuwa na uchakavu mkubwa wa vyumba vya madarasa, na shirika hilo lilipoona shida hiyo, walianza kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, na baadae kujenga tenki la lita 50,000 la kuhifadhi maji ya mvua, na sasa wamejenga vyoo vya kisasa kwa wanafunzi.
Akisoma taarifa ya shule kwa niaba ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Masatu,
Zalka Amiri, Mwalimu, Saleh Kanju amesena wanalishukuru shirika hilo kwa kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa na amani baada ya kupata miradi ya madarasa, maji na matundu ya vyoo.

“Kabla ya Shirika la World Vision kutujengea vyumba viwili vya madarasa, baadhi ya wanafunzi walikuwa wanasoma chini ya mti, lakini tunashukuru hivi sasa wanafunzi wote wanasoma wakiwa darasani. Pili, mradi wa vyoo, tena vyoo vya kisasa. Kabla ya kujengewa vyoo na Shirika la World Vision, shule ilikuwa na uhaba wa vyoo, kwani vilivyokuwepo vilikuwa havitoshi, lakini leo tunasema aksante World Vision, tena tunawapa kongole. Na tatu ni mradi wa maji ambao utanufaisha wanakijiji wote.
“Pamoja na shukrani tulizotoa, pia shule ina changamoto ikiwemo uhaba wa Ofisi ya Walimu, ukarabati wa vyumba vya madarasa, choo cha walimu, kwani walimu wanatumia tundu moja jinsia zote, na uhaba wa jiko” amesema Kanju.
Akisoma taarifa ya makabidhiano ya miradi hiyo, Mratibu wa Mkumburu AP Daniel Chuma amesema miradi ya Maji, Usafi na Usafi wa Mazingira (WASH) yenye thamani ya sh. milioni 349
Mkumburu AP ni mradi wa maendeleo ya jamii unaofadhiliwa na World Vision Hongkong. Mradi umeweka mkazo mkubwa zaidi katika kuboresha maisha ya jamii na haswa watoto.

“Mradi ulianza Oktoba 2013 na unatarajiwa kufikia kikomo Septemba 2031.Katika kipindi cha uhai wa mradi, mradi unashirikiana na Serikali na wadau wengine na kutekeleza miradi kwenye nyanja za kilimo , ufugaji, uhakika wa chakula, elimu, afya, lishe, maji na nyanja zingine mtambuka. Mradi unatekelezwa katika vijiji vinane (8), kwenye kata tatu za Kwamgwe, Kwedizinga na Segera.
“Katika kuboresha usafi, na upatikanaji wa maji safi kwa watoto shuleni, Mkumburu AP ilibua mradi wa vyoo ,vitakasa mikono na uvunaji wa maji ya mvua. Mradi huu ulitekelezwa katika shule 11. Mradi huu ulitekelezwa na World Vision Tanzania kwa kushirikiana na jamii na halmashauri, kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla” amesema Chuma.

Chuma amesema miradi Iliyotekelezwa
ni ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Masatu, matundu: 12 (wavulana na wasichana) kwa gharama ya sh. milioni 89, ambapo wanufaika ni wavulana 330
na wasichana: 343 jumla 673. Mradi wa uvunaji maji ya mvua na vitakasa mikono
matenki manane (8) (lita 50,000 kila moja katika shule nane (8) za msingi),
vitakasa mikono vitano (shule nne (4) za msingi na moja ya sekondari),
jumla ya gharama sh. 260,104,555, ambapo wanufaika:wavulana ni 3,064, wasichana 2,605, wanaume 45 na
wanawake 76, jumla 5,790.



“Nyumba ya mitambo na Solar, Mradi wa Maji Kijiji cha Masatu unaojengwa kwa ufadhili wa World Vision na kusimamiwa na RUWASA , umefikia asilimia 80.”


More Stories
RC akemea uvuvi haramu
Usimikaji mitambo hewa tiba wamkosha Kihongosi
Skimu za Umwagiliaji zinavyopeleka furaha kwa Wakulima Mbarali