January 19, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB,IFAD wazungumzia kuwawezesha mitaji wakulima wadogo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo(IFAD) wameunganisha nguvu ili kuwawezesha mitaji wakulima wadogo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao sambamba na kukuza kipato cha wakulima hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na Mwakilishi Mkazi wa IFAD Tanzania, Jacquline Machangu, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema wamekuwa na mazungumzo yenye yenye tija kwa manufaa ya nchi kwa kuwawezesha wakulima mitaji ili wafanye kilimo cha kibiashara.

“Tutaendelea kushirikiana na IFAD kuhakikisha wakulima wadogo wanapata mitaji itakayo wawezesha kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao hali itakayochochea maendeleo kwa wakulima na uchumi wa nchi kukua,” amesema Nyabundege

Ameeleza kuwa TADB inasimamia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) kwa niaba ya Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, fedha zinazosimamiwa na TADB kupitia mfuko wa SCGS ni dola za marekali milioni 25 kutoka IFAD.

“Kupitia ufadhili huu TADB imeweza kuwafikia moja kwa moja wakulima wadogo 11,468 na kuwafikia wakulima mmoja mmoja zaidi ya 766,380, Tunashukuru ushirikiano mkubwa ambao IFAD wanautoa kwa Serikali nakufanya malengo ya Serikali katika kuwahudumia wananchi wake yaweze kufikiwa,”alisema Nyabundege

Alieleza kuwa TADB inaendelea kufanya kazi kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha ya wakulima kupitia kuwawezesha kimitaji. Ili kufikia hayo tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa kama IFAD kwa kupata fedha zitakazowezesha kuboresha hali za wakulima.

“TADB kwa sasa inashirikiana na taasisi 12 za kifedha katika kutekeleza Mfuko wa SCGS ambapo umewezesha kuboresha hali za wakulima wadogo kwa kupata mikopo ya kuendeleza shughuli za kilimo kwa dhamana ya TADB,” alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania(TADB)Bw.Frank Nyabundege(kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa maendelo ya Kilimo(IFAD) Tanzania, Bi.Jacqueline Machangu(kulia) alipotembelea ofisi za mfuko huo mwishoni mwa wiki na kufanya mazungumzo ya namna ya kuwawezesha mikopo wakulima wadogo nchini.

Aidha, Nyabundege ameeleza kuwa Benki yake inatoa mikopo ya kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ikiwa ni kuongeza ubora zao kwenye mnyororo mzima wa thamani wa mazao hali itakayomfanya mkulima kupata soko la uhakika la mazao yake mara baada ya mavuno.

“TADB imetumia mfumo huo ili kuwawezsha wakulima wengi ambao wanachangamoto ya masoko ya kuuza mazao yao, hivyo upatikanaji wa masoko kutawawezesha wakulima kuwa na hamasa ya kufanya kilimo na baada ya kuuza waweze kujikimu wao na familia zao, “amesema Nyabundege

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa IFAD Tanzania, Jacquline Machangu aliipongeza TADB kwa kazi nzuri wanayofanya kuhakikisha wakulima wanafikiwa na huduma za kifedha ili kuwezesha sekta ya kilimo kupiga hatua.

“Ninaelewa kuwa bado kuna changamoto katika upatikanaji wa fedha, hata hivyo napongeza kazi iliyofanywa na taasisi yenu. Aidha nimejifunza kuwa kuptia TADB mmeweza kushawishi kiwango cha riba katika sekta ya kilimo kupungua hii itawezesha wakulima kupata mikopo kwa riba nafuu zaidi,” amesema Machangu

Ameeleza kuwa Wakulima wadogo nchini Tanzania wanalima hekta ardhi 5.1 na kuzalisha asilimia 85 ya chakula cha nchi. “Hii ndiyo sababu IFAD inafanya kazi bila kuchoka na Serikali ya Tanzania. Ikiwa tunataka kuona Tanzania inamaliza njaa, kutokomeza umaskini, kuboresha maisha na lazima wakulima wadogo waweze kufikiwa na kupatiwa mikopo ili waendeleze kilimo,”amesema.

TADB na IFAD wamedhamiria katika kuongeza juhudi za kuwafikia wakulima wadogo katika maeneo yote nchini ili waweze kupatiwa elimu katika kufanya kilimo cha kibiashara sambamba na kuwapatia mikopo itakayowawezesha kufanya kilimo chenye tija.