April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwekeza kurahisisha mitihani mtandaoni

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuendelea kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa mtandao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwasili katika viwanja vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwa ajili ya kushiriki kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza hilo Jijini Dar es Salaam leo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) iliyofanyika katika Ofisi za Baraza hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu serikali imefanya uwekezaji katika TEHAMA ambao umeimarisha utendaji wa Baraza na kuongeza matumizi ya teknolojia katika usajili wa watahiniwa, uchapaji na usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.

Taarifa hiyo ilimkariri Rais Samia akisema ‘Serikali itaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu ili kuhakikisha ufundishaji, usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria Maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) yaliofanyika katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam leo.

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na NECTA kutafuta mkakati wa kushughulikia changamoto ya udanganyifu wa mitihani.

Aidha, Rais Samia pia amelitaka Baraza la Mitihani kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususan katika upimaji wa umahiri.

Rais Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa Baraza kulingana na mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana na Baraza hilo ili lifikie malengo ya muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapaji kadri uwezo utakavyoruhusu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiwa amenyanyua juu Tuzo ya Shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) yaliofanyika katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea kitabu cha miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza hilo katika Ofisi za Baraza hilo Jijini Dar es Salaam leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi wa Chapa na Uchapishaji kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Edward Haule kuhusu shughuli mbalimbali za uchapaji wa Mitihani pamoja na Nyaraka mbalimbali wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza hilo Jijini Dar es Salaam leo.