May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safari ya wanawake kuwania nafasi za uongozi bado mlimani-wanaharakati

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

LICHA ya kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi bado wanawake wameshidwa kutojitokeza kuwania nafasi mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa na Jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mtendaji wa
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi, wakati akisoma tamko Kwa niaba ya Mtandao wa Bajeti yenye Mtizamo wa Kijinsia,Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini Tanzania (TAMWA), Ushiriki Coalition pamoja na
Taasisi ya Vyombo vya Habari kusini mwa Afrika (Misa-Tan), wakati wakisherekea siku ya wanawake katika kuelekea siku ya wanawake Duniani Machi 8

“kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa ‘Wekeza kwa Wanawake, Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”

Liundi amesema ni umuhimu kuwekeza kwa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa ili kuleta maendeleo shirikishi.

Amesema upande wa Wabunge wa kuchaguliwa, idadi ya wanawake ni 24 kati ya Wabunge 264 ambayo ni sawa na asilimia 9.1 huku idadi ya Wabunge wanawake wa viti maalumu ni 113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya Wabunge wote na jumla ya Wabunge wanawake ni 141 sawa na asilimia 37 ya Wabunge wote ambao ni 393.

“Kutokujitokeza kwa wanawake kuwania nafasi mbalimbali ya uongozi katika changuzi mbalimbali kunapelekea kuwepo Kwa idadi ndogo ikilinganishwa na lengo la kufikia asilimia 50/50″amesema Liundi

Akizungumzia upande Madiwani amesema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya Madiwani wanawake wa kuchaguliwa kutoka kwenye kata ni 204 ambayo ni sawa ana asilimia 3.8 ya Madiwani wote huku Madiwani wanawake wa viti maalumu ni 1,407 sawa na asilimia 26.2 ya Madiwani wote.

“Kwa ujumla wa wanawake Madiwani ni 1,611 sawa na asilimia 30 ya Madiwani wote ambao ni 5,353 huku upande wa Serikali za mitaa, mwenyeviti wa serikali ya vijiji wanawake 246 sawa na asilima 2.1, na katika ngazi ya vitongoji, wanawake wenyeviti ni 4,171 kati ya 62,612 ambayo ni asilimia 6.6″amesema Liundi.

Aidha akitaja changamoto inayochangia kurudisha nyuma harakati za ukombozi wa wanawake ikiwemo umiliki mdogo wa wanawake kwenye Ardhi.

“Umiliki wa ardhi na rasilimali:
Umiliki wa ardhi kwa wanaume ni asilimia 75% ukilinganisha na asilimia 27 kwa wanawake wengi wao wanatumia kwa kulima mashamba madogo madogo kwa kuzalisha mazao ya chakula kwa ajili ya familia jambo ambalo linawakosesha muda wa kushiriki katika shughuli za kuwaongezea kipato na kuwatoa kwenye lindi la umasikini kwani wameachiwa jukumu la kulisha familia”amesema Liundi

Pia amesema kwa wanawake kukosa umiliki wa ardhi kumekuwa kukisababisha kukosa fursa mbalimbali ikiwemo mikopo Kwa ajili ya kujikwamua.

Vilevile amesema kwa upande wa upatikanaji wa huduma ya afya, bado kuna changamoto ya vifo vya wanawake wakati wa kujifungua wanawake 238 katika kila wanawake 100,000 hupoteza maisha wakati wa kujifungua, hatujaweza kufikia lengo tulilojiwekea la kupunguza vifo hadi 200 kati ya vizazi 100,000.

” Inasikitisha sana kuona wanawake wanaoleta nguvu kazi ya taifa wanapoteza maisha yao wakati wa uzazi takribani asilimia 20 ya wanawake hujifungulia nje ya huduma rasmi za afya jambo ambalo linahatarisha maisha yao. Asilimia 27 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15-19 wana watoto au ni wajawazito”amesema

Vile vile, amesema uwekezaji wa bajeti katika sekta hii bado ni changamoto, hatujaweza kufikia lengo la makubaliano tuliojiwekea ya Azimio la Abuja la kutenga asilimia 15ya bajeti ya taifa kwa ajili ya sekta ya afya ambapo hadi mwaka 2023/24 kumetegwa asilimia 5.5% ya bajeti yote hivyo bado safari ndefu.

Akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya siku ya wanawake liundi amesema
wamejipanga kuwa na mtiririko wa matukio mbalimbali kuanzia ngazi ya jamii kupitia Vituo vya Taarifa na Maarifa pamoja na kuwezesha mazungumzo rika yanayounganisha wanawake vijana na wanawake wabobevu katika nyanja mbalimbali.

“Tunaposheherekea siku ya wanawake kwa mwaka 2024, tunapata fursa ya kutafakari mafanikio ya harakati za ukombozi wa wanawake, usawa wa kijinsia, tulikotoka, tuliko pamoja na tunapotaka kwenda”amesema Liundi

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya TGNP, Gemma Akilimali amesema
Mojawapo ya jitihada muhimu zinazopaswa kufanywa ni kuchechemua mabadiliko ya sheria na sera hususani mabadiliko ya kikatiba yatakayo weka mazingira wezeshi ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi ya maamuzi.

“Huu ni uwekezaji muhimu sana na unatakiwa kupewa kipaumbele tunatambua juhudi za kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi, hata hivyo bado kuna changamoto nyingi ambazo ni za kikatiba ambazo zinahitaji mabadiliko ya kikatiba na sio sheria moja moja”amesema Akilimali

Aidha amesema uwekezaji kwa wanawake ni fursa hivyo haki za wanawake kama suala la uwekezaji litasaidia katika kutengeneza suluhisho la kimkakati litakalosaidia wanawake kutambua na kupata haki zao, na hivyo kuweza kuondokana na umasikini.

“Kuwekeza kwa wanawake ni msingi wa kujenga jamii jumuishi niwakumbushe kuwa wanawake wakiendelea, jamii nzima inaendelea” alisisitiza Akilimali

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP Lilian Liundi akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki katika Maadhimisho ya siku ya wanawake yaliofanyika katika viwanja vya TGNP mabibo Dar es salaam.
Mwenyekiti wa bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP Gemma Akilimali akizungumza na wadau waliojitokeza katika Maadhimisho ya siku ya wanawake