May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Royal Tour ya Samia yapeleka neema NCAA

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kazi kubwa iliyofanywa
na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake ya Royol Tour
imeongeza kasi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Hayo yamemsemwa jijini Dar es Salaam leo na Kamishna wa Uhifadhi wa
NCAA, Richard Kiiza, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya
habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana wa miaka mitatu ya uongozi wa
Rais Dkt. Samia.

Amesema takwimu za NCAA zinaonesha juhudi za Rais Dkt Samia katika
kufufua sekta ya utalii mara baada ya UVIKO 19 kupitia filamu ya
Tanzania the Royal Tour zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya wageni
wanaotembelea Hifadhi.

Kwa mujibu wa Kiiza idadi ya watalii imefikia 752,232 kwa mwaka wa
fedha 2022/2023 ikilinganishwa na wageni 191,614 waliotembelea Mamlaka
hiyo Mwaka 2020/2021.

“Idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi inatarajiwa kuendelea
kuongezeka zaidi na kufikia wageni 1,000,000 kwa mwaka wa fedha
2023/2024 hususani, katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2023/2024.

Hifadhi imepokea wageni 534,065 idadi hii imeongezeka kwa asilimia
kumi ikilinganishwa na idadi ya wageni walitembelea hifadhi katika
kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023.”Amesema,

Aidha, Kiiza amesema ongezeko la idadi ya wageni limekuwa na matokeo
chanya kwenye ongezeko la mapato yatokanayo na utalii, ambapo mapato
yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka sh.bilioni 31 mwaka
2020/2021 hadi kufikia sh. bilioni 171 mwaka 2022/2023.

Aidha Kiiza amesema mapato yanategemewa kuongezeka zaidi na kufikia takribani sh. bilioni 200 kwa mwaka kwani katika kipindi cha nusu ya
kwanza ya Mwaka 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 123
tayari mapato yameongezeka kwa asilimia 13 ukilinganisha na mapato
yaliyo kusanywa katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2022/23.

Pia Kiiza amesema Rais Samia alitoa pesa za Uviko 19 kiasi sh.
6,645,258,276) ambazo zilitumika kuimarisha miundo mbinu ya barabara
na kununua mitambo pamoja magari makubwa ya kutengenezea barabara,
kuimarisha viwanja vya ndege pamoja na miundo mbinu mingine ya utalii
ili wageni waweze kufikia vivutio vya utalii kwa urahisi.

Aidha amesema Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni sitini na tisa
kwa ajili ya kujenga tabaka gumu kipande cha barabara chenye kilomita
29.5 kutoka lango kuu la kuingilia Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro
hadi Seneto nia ni kuweka tabaka gumu kipande chote cha kiliomita 83
za barabara ya kuanzia lango kuu (Lodoare gate) hadi mpaka wa Hifadhi
ya Serengeti (maarufu kama golini).

Kuhusu zoezi la kuhamisha kwa hiari wananchi wanaoishi katika eneo la
hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Kiiza amesema hadi kufikia tarehe
25.02.2024 jumla ya kaya ambazo zimeshahama kwa hiari kutoka ndani ya
eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni kaya 1042 zenye watu watu
6,461 na mifugo ipatayo 29,919.

Mbali na hayo, Kiiza amesema Mamlaka Mamlaka imeweza kudhibiti matukio
ya ujangili wa wanyamapori (nyamapori na vipusa) katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo katika kipindi husika mamlaka imeweza kudhibiti matukio ya ujangili wa tembo kutoka matukio 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja mwaka 2022/2023.

“Hii imewezekana kutokana na Serikali kuiwezesha mamlaka kununua
magari ya doria na vitendea kazi vingine, aidha, katika kipindi husika
mamlaka kwa kushirikiana na vikosi vya kupambana na ujangili
ilifanikiwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola
watuhumiwa 175 wanaojihusisha na vitendo vya ujangili,” amesema
Kamishna Kiiza.