April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rena Callist: Maandalizi ‘Miss East Africa 2021’ yashika kasi

Penina Malundo, TimesMajira Online

RAIS wa mashindano ya kumsaka mlimbwende wa ukanda wa Afrika Mashariki ‘Miss East Africa 2021’ yatakayofanyika katika jiji la Dar es Salaam, Tanzania Novemba mwaka huu Rena Callist amesema maandaliai kuelekea kwenye shindano hilo yanakwenda vizuri.

Mashindano hayo yatazishirikisha nchi 16 ambazo ni mwenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somalia, Madagascar, Malawi, Seychelles, Sudan Kusini, Comoros, Reunion na Mauritius.

Kwa mara ya kwanza mashindano hayo yaliyoanzishwa na Mtanzania Rena Callist mwaka 1996 kwa mafanikio makubwa katika Hoteli ya Sheraton (kwa sasa Serena) na pia yamewahi kufanyika katika Nchi ya Burundi kwa udhamini wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati, Piere Nkurunzinza na mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2012 katika ukumbi wa Mlimani City.

Akizungumza wakati alipotembelea maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Tantrade akiambatana na Mabalozi wa mbalimbali wa mashindano hayo wakiwemo Mshindi wa Mashindano hayo kwa mwaka juzi wa nchini Rwanda, amesema tayari maandalizi ya awali yalishafanyika na sasa wanaendelea na maandalizi mengine ili nkuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ubora wa hali ya juu.

Amesema, lengo la kutembelea maonesho hayo ni kuangalia fursa mbalimbali
ambazo wanaweza kuzitangaza kupitia mashindano yao ya Miss Afrika ambayo yanaonyeshwa Dunia nzima.

Kwa mwaka huu mashindano hayo yanatarajiwa kuangaliwa na watu wengi Dunia nzima kupitia kwenye matangazo ya moja kwa moja ya Televison (LIVE) hivyo yatatoa nafasi nzuri ya kutangaza utalii wa Tanzania pamoja na kuonyesha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

“Hii ni fursa kwa makampuni mbalimbali yanayohitaji kutangaza biashara zao kwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kupitia katika mashindano haya makubwa ya urembo na tayari maandalizi ya awali yameshafanyika na tutahakikisha mashindano haya yanafanyika kwa ubora wa hali ya juu kuliko miaka yote ya nyuma lakini pia itakuwa ni fursa kubwa kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii na kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo,” amesema Rena.

Pia amesema kuwa, kuanzia sasa mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka ambapo yatasaidia katika kudumisha umoja wa Afrika mashariki, kukuza utalii, kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji hasa katika nchi inayoandaa Mashindano hayo na pia kutoa elimu na kusaidia katika changamoto mbalimbali hasa zinazowakabili wanawake na watoto wa ukanda huu wa Afrika ya Mashariki.