June 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yagawa mitungi ya gesi Chamwino

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), umegawa mitungi 50 ya gesi ya kupikia kwa Wafanyabiashara wa huduma za chakula maarufu kama mama lishe na baba lishe katika Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Mitungi hiyo imegawiwa leo, Juni 6, 2026, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Chamwino, hafla iliyoongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi (Mb), amesema wizara yake kupitia REA inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata na kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

“Ukienda katika taasisi mbalimbali zinazohudumia watu zaidi ya 100, tayari matumizi ya nishati safi ya kupikia yameanza kutumika kwa kiwango kikubwa. Serikali imejipanga kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaongezeka katika sekta zote,” alisema Ndejembi.

Aliongeza kuwa wakati Rais Samia alipozindua kampeni ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia, kiwango cha matumizi ya nishati hiyo kilikuwa asilimia 6 pekee, lakini kwa sasa kimeongezeka na kufikia asilimia 24, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Wizara ya Nishati pamoja na REA kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisema hatua hiyo itasaidia kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.

Baadhi ya mama lishe na baba lishe waliopokea mitungi hiyo ya gesi waliishukuru REA kwa msaada huo, wakieleza kuwa utawasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika shughuli zao za kila siku, jambo ambalo litapunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuchangia katika uhifadhi wa mazingira.