May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akifungua leo maonesho ya Nanenane Kanda ya Magharibi yaliyofanyika katika Viwanja vya Ipuli katika Manispaa ya Tabora.Picha na Vincent Tiganya

RC Tabora ahimiza WECTU kuwasaidia wakulima kusonga mbele

Na Tiganya Vincnt, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt.Philemon Sengati amekitaka Chama Kikuu Cha Ushirika Cha Wakulima Wa Tumbaku Kanda Ya Magharibi (WETCU Ltd) kuhakikisha kinawasaidia wakulima wake kuwa na uzalishaji bora wa mazao ili waweze kusonga mbele na kuishi maisha mazuri,

Alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora wakati alipotembelea banda la WETCU katika maonesho ya nane nane kwa kanda ya magharibi inayojumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma.

Dkt.Sengati alisema WETCU inajukukumu la kuhakikisha wakulima wake wanatumia mbegu bora na teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo tumbaku ili waweze kupata tija kubwa.

Aliongeza kuwa ni vema wakulima hao wakatumia elimu inayotolewa katika maonesho ya nane nane kujifunza na kuchukua mbinu za matumizi ya mbegu bora za kilimo kuongeza uzalishaji kwa ajili ya maendeleo yao.

“Ni vema tuwahimize wakulima waje nane nane kwa ajili ya kuchota ujuzi na teknolojia mbalimbali inayotolewa hapa kwa ajili ya kuongeza tija kwa uzalishaji wa mazao bora na mengi ambayo yatawasaidia kujenga nyumba bora, kula vizuri na kusomesha watoto wao” alisisitiza.

Aidha mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alisema wakati mazungumzo na wadau mbalimbali ili waweze kujenga kiwanda mkoani Tabora ambacho kitasindika tumbaku kwa ajili ya uzalishaji bidhaa zinazotokana na tumbaku.

Alisema lengo ni kutaka wakulima waongeze uzalishaji na kuondokana na tumbaku yao kubaki kutokana na kupewa makisio ya chini na wanunuzi.