January 19, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Ruvuma ashauri wafugaji watafutiwe maeneo ya kuchungia mifugo yao

Na Cresensia Kapinga, TimesMajira,Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na wadau wa maendeleo, wakiwemo viongozi wa halmashauri, Chama cha Wafugaji, pamoja na wataalam kuwatafutia wafugaji maeneo ya kuchungia mifugo yao.

Amesema wafungaji wamekuwa wakihamahama jambo ambalo linachangia migogoro baina yao na wakulima pamoja na watumiaji wengine wa ardhi.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema, ambaye alimwakilisha Brigedia Jenerali Ibuge wakati akifungua mafunzo ya siku moja ambayo yametolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuhamasisha utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo katika Mkoa wa Ruvuma.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Songea Club Manispaa ya Songea.

Amesema kwa Mkoa wa Ruvuma kuna wimbi kubwa la uingiaji wa mifugo, jambo ambalo linapelekea kuwepo viashiria vya migogoro baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Kwa msingi huo, alisema mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuondoka viashiria hivyo baada ya kuwapa elimu wafugaji.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema akisoma taarifa kuhusu mafunzo ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Songea Club Manispaa ya Songea.

“Nitoe wito kwa Wizara ione umuhimu wa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, viongozi wa halmashauri, chama cha wafugaji pamoja na wataalam ili kutatua changamoto hiyo, kwani wafugaji wengi hawana maeneo ya kuchungia hali inayopelekea kuwa na utaratibu wa kuhama hama na kusababisha migongano baina ya wakulima, wahifadhi pamoja na watumiaji wengine wa ardhi,” alisema Mgema.

Amesema ili kutatua changamoto hiyo ni pale ambapo mkulima atakuwa na sehemu ya kulima na mfugaji atakuwa na sehemu ya kufugia kwa kuwatengea wafugaji maeneo ambayo yatasaidia zoezi la utambuzi wa mifugo kufanyika kwa ufanisi na urahisi.

Mgema amesema kuwa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ni mfumo unaowezesha kuwa na alama na kumbukumbu ya mifugo kupitia usajili wa mifugo yenyewe, wamiliki wake, mahali ilipo na matukio muhimu kwenye uhai wa mifugo na kwamba taarifa za usajili na uchukuaji wa taarifa za mnyama, mfugaji au mahali na kuzihifadhi kwa njia ya kieleketroniki na kuzitoa pindi zitakapo hitajika kwa madhumuni mbalimbali.

” Awamu ya kwanza zoezi la utambuzi kwa njia ya chapa ilikuwa na mapungufu mengi, moja wapo wataalam wetu hawakupata muda wa kupata mafunzo ya kutosha na hata vifaa vya chapa havikuwa na ubora hivyo ilipelekea uharibifu wa ngozi za wanyama kwani baadhi ya Mifugo walipata vidonda na chapa yenyewe haikuwa ya kudumu kwa muda mrefu na kusababisha ubora wa ngozi zilizozalishwa kuwa mbovu” amesema Mgema.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku moja ya zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo yaliyotolewanna Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa wakuu wa Wilaya,wakurugenzi, wataalam na wawakilishi wa wafugaji mkoani Ruvuma.

Aidha amewataka washiriki wa mafunzo hayo ya awamu ya pili ya utambuzi wa mifugo kuwa utafanyika kwa teknolojia ya kisasa ambayo ni kuweka heleni ambazo zitakuwa zikisajiliwa kwa njia ya kisasa ya mtandao, hivyo wadau wote wa sekta ya mifugo kushiriki kikamilifu katika kuwatambua na kuwasajili wafugaji wote waliopo mkoani humo.

Kwa upande wao washiriki hao waliipongeza Wizara kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatasaidia kudhibiti wizi wa mifugo, kuthibitisha umiliki wa mifugo,lakini fursa za kibiashara kimataifa kwa kukidhi viwango vya ushindani na matakwa ya soko la kimataifa pia itasaidia kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Jamii ya Mifugo, Stanford Ndibalema amesema mafunzo hayo yatasaidia kuweka kumbukumbu sahihi za idadi ya wanyama waliopo kwenye mkoa husika na kuepukana na migogoro isiyokuwa na tija baina ya wafugaji na wakulima.