May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kinara utekelezajiwa miradi ya maendeleo-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara na kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoigusa jamii ya Watanzania.

Amesema kuwa maono na misingi iliyojengwa na Rais, Dkt. Samia imewezesha Serikali ya awamu ya sita kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.

“Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha usafiri wa anga, usafirishaji kwa njia ya reli, barabara na usafiri katika bahari na maziwa makuu”.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakitazama daraja la JPM lililopo Kigongo-Busisi ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 42 wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo pamoja na kivuko cha Mv.Sengerema na Mv.Misungwi.

Amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa Kongamano wa Maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia lililofanyika Mkoani Mwanza.

Aidha, alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya usafiri katika maziwa makuu Serikalk imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori matatu na hadi sasa umefikia asilimia 94 ya ujenzi wake.

Amesema sambamba na ujenzi wa meli katika maeneo mbalimbali, Serikali pia imefanya maboresho katika bandari na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari hizo ikiwemo bandari kwenye Ziwa Victoria.

Ameongeza kuwa katika kuimarisha Sekta ya kilimo, Serikali imeendelea kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma kwa kuongeza Bajeti katika Wizara ya Kilimo.

“Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa zao la Pamba ikiwemo kuongeza thamani ya zao hili nitoe wito kwa wakulima wa zao hili kuongeza uzalishaji ili mahitaji tuliyonayo yaendane na uhitaji uliopo”.

Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi pamoja na kutoa zana bora, pembejeo na vifaa muhimu vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi lengo ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwemo utekelezaji wa

“Katika kuimarisha Sekta ya uvuvi Rais amewezesha kununuliwa na kusambaza boti 160 za kisasa za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni 11.5 kwa vyama vya ushirika wa wavuvi, watu binafsi na vikundi vya wavuvi katika Halmashauri 58.”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizowekwa na Serikali ya awamu ya sita ili kukuza uchumi wa Nchi na uchumi wao binafsi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo alisema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha Sekta ya elimu, afya na miundombinu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jukwaa la Mafiga Matatu, Aloyce Nyanda amesema kongamano hilo ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa miradi uliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania nzima kwa ujumla.

Kongamano hilo limehudhuriwa na watu wa kada mbalimbali ikiwemo wabunge, wahadhiri, watumishi wa Serikali, wafanyabiashara na wanafunzi wa vyuo mbalimbali jijini Mwanza ambao walipata nafasi ya kuchangia mada na kuuliza maswali.