May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko akagua matengenezo mashine za kufua umeme Kidatu

*Aigaza TANESCO kutafuta mwarobaini tatizo la kufeli kwa Gridi mara kwa mara

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amefanya ziara ya dharura katika Kituo cha kufua umeme cha Kidatu, Mkoani Morogoro kufuatia kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa jana usiku na kusababisha mikoa mingi Tanzania Bara na Zanzibar kukosa huduma ya umeme.

Dkt. Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linatafuta suluhisho la kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa mara kwa mara.

Aidha, amewataka TANESCO kuhakikisha wanafanya upembuzi wa kina ili kuboresha miundombinu kwenye Gridi na kuongeza kuwa matatizo kama hayo yanapojitokeza yawe funzo yasijitokeze tena.

“Nawaomba radhi sana wananchi na watanzania kwa ujumla kufuatia hitilafu hii kwenye mfumo wa Gridi, kwani imeleta usumbufu na changamoto kwa wananchi kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama” alisisitiza Dkt. Biteko.

Aliongeza kuwa, vipato vya wananchi vinategemea zaidi uwepo wa nishati ya umeme hivyo TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo wakati wote.

Dkt. Biteko amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo-Hanga kwa kuchukua hatua za haraka kufika kwenye eneo la changamoto bila kusukumwa bali kwa kujiongeza.

Aidha, Dkt Biteko, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, kuhakikisha timu yote ya wataalamu inashirikiana ili kupata suluhu ya changamoto hiyo ya umeme na kuiondoa kabisa.

Pia, amewatahadharisha TANESCO kuchukua tahadhari hususan katika kipindi hiki cha kiwango kikubwa cha mvua zinazonyesha na kuwataka TANESCO kuchukua tahadhari.

Amesema, maji yanayoingia kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ni kikubwa na kutolea mfano wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere ili kuondoa madhara yanayoweza kusababishwa na wingi wa maji hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Danstan Kyoba amewashukuru Wizara ya Nishati kwa hatua ilizochukua kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa wakati.

Amewatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari kufuatia kiwango kikubwa cha mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kuharibu miundombinu mbalimbali.