May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkeka wa Samia mchungu, mtamu Sikukuu ya Pasaka

*Makonda apelekwa kwa Lema Arushaa, Mongella awekwa benchi, Prof Ndalichako ‘OUT’ Baraza la Mawaziri, azidi kufoka kwa kalamu

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho, uteuzi na ametengua baadhi ya viongozi mbalimbali, ambapo mkeka wake huo ulitangazwa jana kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Mkeka huo, umewafanya baadhi ya walioguswa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kicheko, huku wangine wakiwa wameinamisha vichwa chini, kutokana nafasi zao kutenguliwa, au kubadilishwa kutoka nafasi walizokuwa wakishikilia awali.

Miongoni mwa walioguswa ni pamoja namawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya. Aidha, mkeka huo wa Rais ambao umetolewa katika Sikukuu ya Pasaka jana, umemgusa pia Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Makonda sasa anenda mkoani Arusha kwenye mkoa ambao ni ngome ya CHADEMA ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ambaye mara kadhaa amekuwa akitoa tuhuma mbalimbali dhidi ya Makonda.

Makonda ametumikia nafasi hiyo kwa muda usiozidi miezi mitano, akiwa amejipatia umaarufu kwa stahili yake ya kutatua kero za wananchi akiwa majukwaani kwenye mikoa 23 aliyofanya iliyopewa jina la Back 2 Back.

Paul Makonda

Katika nafasi hiyo, pengine Makonda ameingia kwenye rekodi nyingine ya kutumikia nafasi hiyo kwa muda mfupi, huku wananchi wengi wakiwa na shauku naye kwa jinsi alivyokuwa akitatua kero zao hasa za ardhi.

Makonda aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Oktoba 22, 2023 akichukua nafasi ya Sophia Mjema.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemuweka pembeni kwenye baraza la Mawaziri Profesa Joyce Ndalichako , ambaye alikuwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Rais Samia amemteua Deogratius Ndejembi aliyekuwa Naibu Waziri wa Tamisemi kuwa waziri Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, akichukua nafasi ya Ndalichako.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia ni kama ifuatavyo. Rais amemteua Deogratius Ndejembi, kuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).
Kabla ya uteuzi huu.

Kabla ya hapo, Ndejembi alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambapo anachukua nafasi ya Prof Ndalichako .

Profesa Joyce Ndalichako

Amemteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambapo kabla ya uteuzi huu, Makonda alikuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na
Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Makonda anachukua Anachukua nafasi ya John Mongella ambaye atapangiwa kazi nyingine. Aidha, amemteua Kanali Evans Mtambi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na kabla ya uteuzi huu, Kanali Mtambi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.

Rais Samia amemhamisha, Said Mtanda kutoka Mkoa wa Mara
kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mtanda anachukua nafasi ya Amos Makalla ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Pia, amemteua Zainab Katimba kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Zainab anachukua nafasi ya Ndejembi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri.

Aidha, amemteua Daniel Sillo kuwa Naibu Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi. Sillo anachukua nafasi ya Jumanne
Sagini , ambaye amehamishwa kwenda kuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Katiba na Sheria.

Mwingine aliyehamishwa Mhandisi Maryprisca Mahundi kutoka
Wizara ya Maji kwenda kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Amemhamisha Kundo Mathew kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na pia amemteua, Fakii Lulandala kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro.

Kabla ya uteuzi huu Lulandala alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). Uteuzi mwingine umemhusu, Gilbert Kalima kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga. Kabla ya
uteuzi huu Kalima alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya
Chama cha Mapinduzi.

Rais Samia amemhamisha Mhandisi Cyprian Luhemeja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu) kwenda kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na pia amemhamisha Mary Maganga kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwenda kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Alimteua Dkt. Edwin Mhede kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi. Dkt. Mhede aliwahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Dkt. Mhede anachukua nafasi ya Agnes Meena ambaye
amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji.

Pia amemteua Dkt. Suleiman Hassan Serera kuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huu Dkt. Serera alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.

Dkt. Serera anachukua nafasi ya Nicholaus Mkapa ambaye
amehamishwa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Mawasiliano na Teknolojia wa Habari.

Rais Samia, pia amemteua Selestine Gervas Kakele kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huu Kakele alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Balozi Dkt. Asha Rose Migiro kuwa Mjumbe wa Tume ya Mipango. Uapisho wa Waziri, Wakuu wa Mikoa, Naibu Mawaziri na Naibu Makatibu Wakuu utafanyika Aprili 4, mwaka huu.