August 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetangaza kuwa lipo tayari kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union – IPU), utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, ukitarajiwa kukutanisha washiriki takribani 2,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza jana jijini Arusha kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kuwapokea wajumbe kutoka mabunge ya nchi wanachama wa IPU pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Spika Zungu amesema ni fahari kwa Tanzania kuwa kwa sasa Rais wa IPU ni Mtanzania, Dkt. Tulia Ackson, ambaye ameshika nafasi hiyo tangu mwaka 2023 na ameendelea kuiongoza taasisi hiyo katika kuimarisha ushirikiano wa mabunge duniani.

Ameeleza kuwa kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni ishara ya imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa ya mabunge inayo kwa Tanzania pamoja na kuthibitisha mchango wa nchi katika kuendeleza demokrasia, amani, ushirikiano wa kimataifa na diplomasia ya kibunge.

Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujumuisha Maspika wa Mabunge, Wabunge, Maafisa wa Mabunge, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na kikanda, wanadiplomasia, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu ya juu pamoja na wanahabari kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Katika mkutano huo, viongozi hao watajadili masuala mbalimbali yanayoigusa dunia kwa sasa, ikiwemo utawala wa kidemokrasia, amani na usalama, mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya kidijitali, matumizi ya akili unde, ushiriki wa watu wenye ulemavu, vijana na wanawake, ustahimilivu wa uchumi pamoja na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Kwa mujibu wa Spika Zungu, majadiliano hayo yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, zikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kimataifa na changamoto za kiuchumi, huku yakionyesha umuhimu wa diplomasia ya kibunge katika kujenga makubaliano na ushirikiano kati ya mataifa.

Mbali na ajenda rasmi za mkutano, Tanzania inatarajia kunufaika kiuchumi kupitia ongezeko la shughuli za utalii, usafirishaji, huduma za malazi na biashara, sambamba na kupata fursa ya kutangaza vivutio vyake vya utalii, urithi wa utamaduni na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wageni watakaohudhuria.

Spika Zungu amesema mkutano huo pia utakuwa nafasi ya kuionesha dunia taswira ya Tanzania kama taifa lenye amani, ukarimu na mazingira rafiki kwa uwekezaji na utalii.

Amebainisha kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kupitia ushirikiano kati ya Bunge la Tanzania, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sekretarieti ya IPU na wadau mbalimbali, huku mipango ikiwa imejikita katika kuhakikisha huduma zote muhimu, zikiwemo usajili, usalama, usafiri, malazi, afya, tafsiri na huduma kwa vyombo vya habari zinakuwa katika viwango vinavyokubalika kimataifa.